November 24, 2024

Video zinazoongoza kwa kutokupendwa YouTube hizi hapa

Zipo video za muziki, video za maudhui kwa ajili ya watoto na video zingine za burudani.

  • Video ya kwanza ambayo imepata dislike nyingi zaidi ni  Video ya YouTube Rewind ya mwaka 2018.
  • Video mbili zilizoingia tano bora zimepakiwa mtandaoni humo kwa kutumia akaunti ya YouTube.
  • Video zilizo na maudhui ya watoto na video zingine za ajabu zimechuana vilivyo kiungia katika orodha hii.

Dar es Salaam. Mtandao wa YouTube ni kati ya mitandao mikubwa iliyosheheni maudhui mbalimbali yakiwemo ya filamu, Muziki, masomo na vichekesho.

Kila mtu huingia katika mtandao wa YouTube akiwa na lengo lake na kwa baadhi, ni kusikiliza muziki na kupata burudani ama kujifunza kitu fulani.

Licha ya mtandao huo kuwafurahisha wengi, wapo ambao  hawafurahishwi na baadhi ya maudhui yanayotolewa na fanani wa mtandao huo.  

Ndani ya mtandao huo, mtu ana uwezo wa kubonyeza kitufe cha kidole gumba kinachoelekea juu (like) ama kidole kinachotazama chini almaarufu kama “dislike” kuonyesha kutokufurahishwa na video aliyoitazama.

Zipo video nyingi ambazo zimejizolea dislike za kutosha lakini hizi ni video 10 ambazo zinaongozwa kwa kutokupendwa na watu katika mtandao huo duniani hadi kufikia leo Februari 13, 2021:

Kwa haraka kabla  ya kuingia tano bora, nafasi ya 10 inashikiliwa na video ya It’s Everyday Bro yake Jake Paul ambayo watu milioni 5.1 hawakuifurahia na watu milioni 3 tu ndio waliiipenda.

Video ya tisa ni “Can This Video Get 1 Million Dislikes” yake PewDiePie ambayo ilizidi ombi la video hiyo la kupata  dislike milioni moja na kupata dislikes milioni 5.17.

Namba nane inashikiliwa na video ya “Flores” yake Vitão na Luísa Sonza yenye dislikes milioni 5.5 huku namba saba ikishikiliwa na video ya “Bath Song” yake msanii Cocomelon iliyo na dislikes milioni 6.1. 

Namba sita inashikiliwa na video ya Johny Johny Yes Papa ambayo ina maudhui kwa ajili ya watoto. Video hiyo imepata dislike milioni 8.9.

Video mbili zilizoingia tano bora zimepakiwa mtandaoni humo kwa kutumia akaunti ya YouTube. Picha| Google Images.

Hali ilivyo katika tano bora ni kama hivi;

05. Video ya “YouTube Rewind 2019”

Hii ni video ya pili iliyopakiwa na mtandao wa YouTube ambayo haijawafurahisha hadhira wake. Video hiyo imepata dislike milioni 9.4 huku ikifurahisha watu milioni 3.4 tu. 

Awamu hii, baada ya kukoselewa katika video ya mwaka 2018, Youtube, iliamua kukata vipande vipande vya watengeneza maudhui na kuviweka katika video  hiyo.

Bado haikutosha kwa hadhira wake.

04. Video ya Baby Shark 

Hii ni video iliyopakiwa na PinkFong! Kids’ Songs & Stories na maudhui  yake ni ya kuwafurahisha watoto.

Hata hivyo, bado haifahamiki kama watoto hawaipendi video hii au ni wazazi wao kwani imejizolea dislike milioni 11 na watu milioni 25 wamefurahishwa na video hiyo ambayo ipo Youtube tangu Juni18, 2016.

Ajabu ni kuwa video hiyo ni miongoni mwa video zinazopendwa zaidi na watumiaji wa YouTube. Ni sawa na kusema wanaipenda sana na kuichukia sana.


Soma zaidi:


03. Video ya muziki wa “Baby” 

Ni yake Justin Bieber akishirikiana na Ludacris iliyotoka tangu Februari 19, 2010. Mwaka huo kama ulikuwa na kifaa cha kusikiliza muziki, bila shaka wimbo huu unaukumbuka,

Licha ya kusumbua spika nyingi, wimbo huo umepata dislike zaidi ya  milioni 12. Kwa wengi na ni ngumu kuchukua upande kwani bado watu milioni 16 wameupenda sawa na tofauti ya milioni 4.

Je, wewe unafikiri ni muziki mzuri au vipi?

 02. Trela ya video ya Sadak sehemu ya pili

Wanaohusika na upakiaji wa video hiyo ni studio za Fox Star na ilikuwa mtandaoni humo kuanzia Agosti 12, 2020. Kisichowafurahisha wengi kuhusiana na video hii ni uwepo wa mwigizaji Alia Bhatt ambaye ni mtoto wa mwongoza filamu za Bollywood (director) Mahesh Bhatt.

Wengi walikereketwa na undugu unaoendelea ndani ya tasnia ya filamu za kihindi hivyo kuungana na kuipatia dislike milioni 13.37 huku waliofurahishwa nayo wakiwa ni watu 737,000 tu hadi leo.

01. Video ya YouTube Rewind ya mwaka 2018

Video hiyo imepakiwa mtandaoni humo na Youtube ikiwa na lengo la kuwatambua watengeneza maudhui waliofanya vizuri zaidi kwa mwaka 2018. 

Hata hivyo, nanga ya video hii haikuweza kunasa sakafu ya hadhira ya Youtube kwa mwaka huo kwani hadi kufikia leo, inaongoza kwa kuwa na dislikes 18 milioni.

Wengi hawaupendi mpangilio wa video hiyo licha ya YouTube kujitahidi kuonyesha maudhui yaliyobamba mwaka huo ukiwemo wimbo wa msanii Cardi B wa “I like it”, na wimbo wa Drake na challange yake ya “Kiki do you love me”.