October 6, 2024

Vigogo watano wa ushirika Tabora jela miaka 4 kwa matumizi mabaya ya ofisi

Wamehukumiwa kwa kununua gari chakavu lenye thamani kubwa kuliko lililopitishwa na Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU) na kukisababishia chama hicho hasara.

  • Wamehukumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, kununua gari chakavu lenye thamani kubwa kuliko lililopitishwa na Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU)na kukisababishia chama hicho hasara.
  • Vigogo hao wa WETCU walikamatwa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupata taarifa kuwa walinunua gari chakavu kwa bei ya gari jipya kinyume na uamuzi wa mkutano mkuu wa chama hicho 

Dar es Salaam. Waliokuwa vigogo wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU), wamehukumiwa kwenda jela miaka minne kila mmoja, baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili likiwemo la kukisababishia chama hicho hasara ya zaidi Sh109 milioni.

Vigogo hao watano ambao walikutwa na hatia mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Tengwa Chiganga watatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani kutokana na adhabu za kifungo chao zinakwenda sambamba.

Waliotiwa hatiani ni aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Mkandala Mkandala; Kaimu Meneja Mkuu, John Kusanja; Mkaguzi wa Ndani, Prosper Mbacho; Mhasibu Mkuu, Francis Mpeta na Makamu Mwenyekiti, Msafiri Ngassa ambao walipelekwa katika gereza la Uyui kuanza kutumikia adhabu zao.

Mahakama hiyo imewaachia huru washitakiwa wawili katika kesi hiyo, Hamza Kapela na mfanyabiashara Faraz Abbas ama Faraz Yaseen Abbasi, kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao pasi na kuacha shaka yoyote.

Washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manne ambayo ni kula njama ya kutenda kosa, kughushi, matumizi mabaya ya madaraka na kununua gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 bila kupata kibali kutoka kwa Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini na kukisababishia chama hicho hasara ya Sh 109.01 milioni kutokana na kununua gari hilo.

Akisoma hukumu hiyo mapema wiki hii, Hakimu Chiganga amesema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa Jamhuri ulileta mashahidi 16 na vielelezo 16 ambapo umeweza kudhibitisha mashtaka mawili bila ya kuacha shaka yoyote dhidi ya washitakiwa Mkandala, Kusanja, Mbacho, Mpeta na Ngassa.

Hakimu Chiganga aliyataja makosa hayo kuwa ni  matumizi mabaya ya ofisi kwa kununua gari chakavu lenye thamani kubwa kuliko lililopitishwa na WETCU na kukisababishia chama hicho hasara.

Akitoa adhabu, Hakimu Chiganga alisema shitaka la kwanza la matumizi mabaya ya ofisi kila mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela na la pili la kukisababishia chama hicho hasara  kila mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela, adhabu ambazo zitakwenda sambamba.


Zinazohusiana: 


Baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili waandamizi wa Serikali walisema hawajaridhika na adhabu hiyo, hivyo waliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufani.

Vigogo hao wa WETCU walikamatwa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupata taarifa kuwa walinunua gari chakavu kwa bei ya gari jipya kinyume na uamuzi wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao uliamuru kununuliwa gari kwa thamani ya Sh40 milioni na mrajisi wa vyama vya ushirika aliridhia.

Inadaiwa washitakiwa hao walinunua gari hilo kwa mfanyabiashara Faraz ambapo nyaraka za gari zinaonyesha ni la mwaka 2008, lakini wao walighushi kadi na kuonyesha ni la mwaka 2014.

Tumbaku ni zao linalotegemewa zaidi na wakulima wa mkoa wa Tabora, hujuma za baadhi ya viongozi zimekuwa kikwazo kwa wakulima kunufaika. Pich| habarizajamii.com

Machi 16, 2017, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimuagiza  Kamanda wa Polisi, Mkoa wa  Tabora kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa  Tumbaku (WETCU) na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

Pia, Majaliwa alivunja Bodi ya WETCU na  Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) kwa kushindwa  kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Alitoa maagizo hayo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora, ambapo pia alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa TTB, Vita Kawawa na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo, Wilfred Mushi.

Majaliwa alisema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na TTB jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.

“Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea Sh15 bilioni ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni Sh10 bilioni ambazo hawajazikatia risiti,” alisema.