November 24, 2024

Vijana nguzo muhimu ya kupigania haki za binadamu-UN

Ikiwa zimepita saa chache tangu dunia iadhimishe siku ya haki za binadamu, Umoja wa Mataifa (UN) umesema mchango wa vijana ni muhimu na wa lazima katika kuhakikisha haki za binadamu ikiwemo uhuru wa kujieleza zinadumishwa kote duniani.

  • Yasema mchango wa vijana ni muhimu na wa lazima katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa.
  • Yataka vijana wanaopigania haki za binadamu walindwe duniani kote.

Dar es Salaam. Ikiwa zimepita saa chache tangu dunia iadhimishe siku ya haki za binadamu, Umoja wa Mataifa (UN) umesema mchango wa vijana ni muhimu na wa lazima katika kuhakikisha haki za binadamu ikiwemo uhuru wa kujieleza zinadumishwa kote duniani. 

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres katika ujumbe wake kuhusu siku ya haki za binadamu inayoadhimishwa Desemba 10 kila mwaka, amesema ulimwenguni kote vijana wana dhamana ya kulinda na kuendeleza haki za watu wote ili kudumisha amani na upendo.

“Kikubwa ni kupaza sauti zao katika masuala ya haki za mazingira, haki sawa kwa wanawake na wasichana, kushiriki katika kufanya maamuzi na kutoa maoni yao kwa uhuru. Wana dhamana kwa ajili ya haki zao na mustakabali wa amani, haki na fursa sawa,” amesema Guaterres katika taarifa iliyotolewa na UN.

Amesisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kupata haki zote za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni bila kujali wanaishi wapi. Pia bila kujali kabila, dini, asili yao, jinsia, mwelekeo wa kijinsia, kisiasa au maoni mengine, ulemavu au kipato, au hali yoyote ile. 


Soma zaidi: Wafanyakazi wengi hawajui haki zao: Ripoti


Katika Siku hiyo ya Kimataifa, Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amemtaka kila mtu awasaidie na kuwalinda vijana ambao wanasimama kidete kwa ajili ya haki za binadamu.

UN Iliteuwa siku hii ili kukumbuka shughuli zote zinazofanywa na wanaharakati wa masuala ya kutetea haki za binadamu, serikali na nchi kwa ujumla, ikiwa ni pamoja kutumia siku hii katika kuhamasisha utekelezwaji wa haki za binadamu.

Desemba 10, 1948 lilitangazwa Azimio na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu Tamko la Haki za Binadamu na tangu mwaka 1950 ilianza rasmi kufanyika Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. 

Tamko hilo lina Ibara 30, ambapo ibara ya kwanza inaeleza kuwa “watu wote wamezaliwa huru hadhi na haki zao ni sawa wote wana akili na wana dhamiri.”