November 24, 2024

Vijana waliopo shuleni watakiwa kuchangamkia fursa za mitaji ya ujasiriamali

Mitaji hiyo itawasaidia kuendeleza miradi wanayoanzisha na kuwaepusha na changamoto za ajira wanapohitimu masomo yao.

Vijana wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupata mafunzo ya jinsi ya kupata mitaji kutoka taasisi ya Anzisha Prize. Picha|Daniel Samson.


  • Mitaji hiyo itawasaidia kuendeleza miradi wanayoanzisha na kuwaepusha na changamoto za ajira wanapohitimu masomo yao. 
  • Pia inawaunganisha na wadau mbalimbali wa maendeleo waliopo ndani na nje ya nchi. 

Dar es Salaam. Vijana waliopo katika shule za sekondari na vyuo vikuu nchini wenye ndoto ya kukuza na kuendeleza miradi ya ujasiriamali wametakiwa kuchangamkia fursa za mitaji inayotolewa na mashirika mbalimbali ili kuongeza wigo wa huduma na soko la kimataifa. 

Fursa hizo zitawatengenezea msingi wa kufanikiwa katika miradi wanayoanzisha na kuwapunguzia mzigo wa tatizo la ajira mara baada ya kuhitimu masomo.

Msimamizi wa miradi kutoka taasisi ya Anzisha Prize, Nolizwe Mhlaba aliyekuwa akizungumza wakati wa kutambulisha fursa zinazotolewa na taasisi hiyo jijini Dar es Salaam juzi (Machi 30, 2019) amesema bara la Afrika lina idadi kubwa ya vijana na inaongezeka kwa kasi, hivyo kuna kila sababu ya wao kutengenezewa mazingira kuwawezesha kujiajiri kwa kuanzisha miradi ya ujasiriamali itakayowasaidia kujikimu kimaisha. 

Amesema vijana wanatakiwa kupewa ujuzi na maarifa wakiwa shuleni ili kuwaandaa kisaikolojia kukabiliana changamoto za kifedha ikiwemo kuwasaidia kupata mitaji ya kuendeleza shughuli za ujasiriamali na kuondokana na dhana ya utegemezi. 

 “Sisi kama Anzisha Prize tunashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuwajengea vijana dhana ya kujiajiri na kuwasaidia kukuza shughuli zao hata kabla hawajamaliza masomo,” amesema Mhlaba. 

Anzisha Prize yenye makao makuu nchini Afrika Kusini  inalenga kuwasaidia vijana wa Afrika wenye umri kati ya miaka 15 hadi 22 wenye mawazo ya kibunifu au biashara zinazosaidia kutatua changamoto za jamii kuendeleza shughuli zao kwa kuwapatia mafunzo, mitaji na uangalizi wa wakufunzi waliobobea katika maeneo husika. 

Pia taasisi hiyo inayoshirikiana na kudhaminiwa na Mfuko wa Mastercard na taasisi ya African Leadership Academy wanahimiza elimu ya ujasiriamali katika shule za sekondari na vyuo vya Afrika ambapo kila mwaka vijana 15 kutoka nchi mbalimbali za Afrika huchaguliwa kuingia katika mafunzo maalum na wote kwa pamoja hupatiwa mtaji wa Dola za Marekani 100,000 (Sh230 milioni) kuendeleza miradi katika maeneo yao.


Zinazohusiana: 


 Asha Abbas ni mmoja wa wanufaika wa Anzisha Prize kutoka Tanzania, anasema kupitia taasisi hiyo amefanikiwa kuanzisha jukwaa la mtandaoni la Aurateen linalotoa nafasi kwa vijana kupata elimu ya afya ya uzazi tangu wakiwa shuleni ili kuwawezesha kufikia ndoto zao kielimu. 

Anasema mafunzo na mtaji wa kuanzisha jukwaa hilo alioupata umemsaidia kuwafikia vijana wengi ambao wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa elimu sahihi ya uzazi. 

Asha ambaye alikuwa miongoni mwa waliopata mafunzo maalum mwaka 2016 kutoka Anzisha Prize anaona hiyo ni fursa kwake kujiajiri na kujihakikishia mafanikio ya ujasiriamali hata baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu.