October 6, 2024

Vijana wanavyopiga madili ya fedha kwa kilimo Morogoro

Mmoja aliyesaka ajira bila mafanikio aweka kibindoni Sh4 milioni kwa miezi minne

  • Ni wale wanaojifunza kilimobiashara katika kituo atamizi katika Chuo Kikuu cha Sokoine. 
  • Mmoja aliyesaka ajira bila mafanikio aweka kibindoni Sh4 milioni kwa miezi minne.

Dar es Salaam. Baada ya kuhitimu Shahada ya Sayansi katika Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2018 na kukosa ajira, Hefsiba Olloo aliamua kugeukia kilimo cha mboga licha ya kuwa shughuli za aina hiyo haziwavutii vijana wengi Tanzania.

Ili kupata maarifa zaidi ya kuongeza tija katika kazi mpya aliyoichagua, Hefsida kijana kutoka Kilimanjaro aliamua kujiunga na Kituo Atamizi cha Vijana cha Kilimobiashara cha Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) Septemba 2019.

Kwa kawaida vituo atamizi maarufu kwa kimombo kama incubators husaidia vijana kupata uzoefu wa kuendeleza ubunifu na biashara walizoamua kuzifanya. Kwa sehemu kubwa nchini Tanzania, viatamizi vingi vimejikita katika kuendeleza biashara au ubunifu unaoegemea zaidi Tehama na mara chache sana kilimo. 

“Kwa muda mfupi tangu nimejiunga na kambi atamizi hapa SUA mwezi Septemba 2019 tayari nimeona manufaa yake kwa kuwa na uhakika wa kipato kupitia kilimo cha nyanya. Nilipanda nyanya mwezi Oktoba mwaka 2019 na sasa naendelea kuvuna” anasema Hefsida.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Kilimo iliyotolewa Aprili 25 mwaka huu ameweza kuzalisha nyanya kwenye kitalu nyumba na kuvuna kilo 1,318 za nyanya zilizompatia Sh4 milioni ndani ya kipindi cha miezi minne.

Katika mavuno hayo, Hefsida alivuna kilo 338 hadi mwisho mwa Januari huku Februari akiweka kibindoni kilo 400 ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi kuliko alichopata katika mwezi wa kwanza mwa mwaka.

Machi alipata kilo 400 na Aprili tayari ameshavuna kilo 180 za nyanya ambazo ameuza zote kwa bei ya wastani wa Sh2,500 hadi 3,000 kwa kilo moja.

Miezi aliyovuna nyanya ni moja ya vipindi ambavyo bidhaa hiyo ilikuwa ikihitajika zaidi kiasi cha nyanya moja kuuzwa hadi Sh500 kwenye maeneo ya mijini kama Dar es Salaam.

Hefsida Olloo (Kushoto) akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ya nanma alivyofanikiwa kuzalisha nyanya katika kitalu kwenye kambi Atamizi ya SUA. Hefsida ni moja ya mabinti wachache Tanzania waliojikita kwenye kilimobaada ya masomo ya elimu ya juu. Picha|Wizara ya Kilimo. 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ameshauri vijana waliohitimu katika vyuo mbalimbali nchini kujitokeza na kupata mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara kwa ajili ya kujipatia ujuzi na ajira toka SUA.

“Vijana tunatambua uwepo wenu hapa kituoni, jitahidini kujifunza mbinu bora za kilimo mkilenga kujiajiri na mwisho wa mafunzo yenu mrudi vijijini na mijini kuwa walimu kwa vijana wenzenu” amesema Kusaya wakati akiongea na vijana wanaondelea na mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara katika kituo hicho.

Kusaya amesema lengo la serikali ni kukifanya kilimo kuwa ni ajira na kazi inayochangia kukuza uchumi wa nchi ndio maana nimekuja kuwatembelea na kuwatia moyo.

Uongozi wa SUA umesema kituo hicho atamizi kinafundisha vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali wanaopenda kufanya kilimo biashara na hadi sasa kuna vijana wapatao 40 wanaoendelea na mafunzo kwa vitendo kwa mwaka mmoja.


Zinazohusiana: 


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Prof Raphael Chibunda amesema vijana hao wanazalisha mazao ya mboga mboga kama hoho za rangi, matango na nyanya kwa usimamizi wa wataalam wa chuo.

Kama ilivyo kwa vituo vingi atamizi vinavyosimamiwa na vijana, kituo hicho kinasimamiwa na kijana Zebedayo Sanga aliyehitimu wa digrii ya masuala ya kilimo cha mbogamboga (Horticulture) mwaka 2018 chuoni hapo.

Sanga amewahamasisha vijana wengi zaidi waliopo mitaani kwenda kujifunza kilimobiashara na kuwa na uhakika wa kipato na ajira kuliko kubaki mtaani wakisaka ajira ambazo zimezidi kuwa adimu siku hadi siku.