November 24, 2024

Vijana wapewa changamoto kujiajiri katika sekta ya nishati jadidifu

Waambiwa sekta hiyo ina fursa nyingi ambazo zikitumiwa kikamilifu zinaweza kuboresha maisha yao na jamii zinazowazunguka.

Vijana kutoka taasisi mbalimbali wakipata mafunzo ya nishati jadidifu Jijini Dar es Salaam. Picha| Zahara Tunda.


  • Waambiwa sekta hiyo ina fursa nyingi ambazo zikitumiwa kikamilifu zinaweza kuboresha maisha yao na jamii zinazowazunguka.
  • Serikali nayo itarahisishiwa kazi ya kusambaza na kuwafikishia umeme wananchi wa vijijini ambao hawajapitiwa na gridi ya Taifa.

Dar es Salaam. Vijana nchini wametakiwa kuchangamkia fursa ya kujiajiri zinazopatikana katika sekta ya nishati jadidifu (Renewable Energy) wakati huu ambao Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inabuni vyanzo mbadala vya nishati ili kuboresha maisha ya wananchi. 

Katika maeneo mbalimbali nchini hasa maeneo ya vijijini bado umeme wa gridi ya Taifa haujafika, jambo linalofungua milango kwa makampuni yanayotoa huduma za umemejua kupeleka vifaa vya sola ili kurahisisha upatikanaji wa nishati mbadala inayochangia katika utunzaji wa mazingira.

KImsingi Vyanzo vya nishati jadidifu ni biashara kubwa duniani – na kwa kawaida ni rafiki wa mazingira, hasa kwa ajili ya kuzuwia mabadiliko zaidi ya tabianchi ambapo hujumuisha jua, upepo, jotoardhi na maji. 

Changamoto hiyo imetolewa na washiriki wa kongamano la siku mbili lililoandaliwa na kituo cha kijamii cha Energy Change Lab kwa kushirikiana na shirika la Hivos East Africa lililowakutanisha vijana zaidi ya 15 kutoka taasisi mbalimbali na wadau wa nishati kujadili na kuangalia ni jinsi gani vijana wanaweza kuwa viongozi wa baadae katika kuipa kipaumbele sekta ya nishati jadidifu ili kunufaika kiuchumi.

“Kwa kweli nimejifunza kwamba sekta ya nishati ni nzuri, vijana tujitoe na tuweke nguvu zetu, kama biashara na kutunza mazingira,” amesema Pius Matunge mmoja wa wanajumuiya kutoka shirika la Raliegh Tanzania.

Washikiri hao wamesema nishati jadidifu inatoa uwanja mpana kwa kijana anayejitambua kutoka sekta yoyote kujifunza mambo muhimu yatakayomsaidia kuikwamua jamii inayomzunguka kwa kutumia nishati ambayo ni muhimu katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.

“Sipo kwenye sekta ya nishati ila nimejifunza vitu na sikuvijua mwanzo kama njia za kupata mawazo mazuri na kuyatumia ili kujinufaisha kiuchumi,” anasema Cornelus Mutuku, Afisa Programu Msaidizi kutoka Hivos East Africa.


Zinazohusiana: 


Katika kongamano hilo vijana wamefundishwa jinsi ya kutengeneza mawazo bunifu na kuanzisha miradi ya inayolenga kuisaidia jamii kuwa na matumizi sahihi ya nishati jadidifu ikizingatiwa kuwa huduma ya nishati mbadala hutolewa na kampuni za kigeni na kuzuia wazawa kunufaika na fursa zinazogunduliwa katika sekta hiyo.

“Vijana wajitokeze kushiriki katika mafunzo kama haya yatawapa mwanga, hata njia iliyotumika kufundishia ni zuri katika kubuni mradi huumii sana,” anasema Adam Mbyallu, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Sahara Venture inayojishughulisha kukuza na kuendeleza ubunifu wa vijana katika teknolojia.

Naye mshiriki kutoka Uholanzi, Mareike Britten amesema  vijana wapo tayari kujihusisha na kufanya kazi bila kutegemea msaada wa fedha za wahisani zaidi ya kujengewa uwezo na maarifa ya msingi ya kuendeleza sekta ya nishati jadidifu katika maeneo yao.  

Ripoti ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati ya mwaka 2016 iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaeleza kuwa mwaka huo theluthi moja (asilimia 32.8) tu ya kaya zote nchini ilikuwa ikipata huduma ya umeme. 

Kati ya kaya hizo zinazopata umeme, tatu kwa kila nne (asilimia 74.9) zimeunganishwa na umeme kutoka katika gridi ya Taifa, takribani robo (asilimia 24.7) zinapata kutoka katika umemejua na asilimia 0.3 tu zinapata umeme kutoka vyanzo vingine vya nishati hiyo.

Takwimu hizo zinadhihirisha wazi kuwa bado idadi kubwa ya wananchi hasa waishio vijijini hawajafikiwa na huduma ya umeme ambapo nishati jadidifu ikitumiwa vizuri inaweza kuwa mkombozi katika maisha yao ya uzalishaji.