November 24, 2024

Vijana wazidi kutawala soko la mitandao ya kijamii Tanzania

Licha ya changamoto za usiri, udukuzi, habari za uongo na mambo mengine hasi ya maisha mtandaoni, bado dunia inaendelea kushikamana na intaneti na mitandao ya kijamii.

Dar es Salaam. Kwa mujibu wa ripoti ya Dijitali ya Januari 2019 iliyotolewa kampuni ya We are social ya nchini Marekani inaeleza kuwa licha ya changamoto za usiri, udukuzi, habari za uongo na mambo mengine hasi ya maisha ya mtandaoni, bado dunia inaendelea kushikamana na intaneti na mitandao ya kijamii. 

Ukuaji wa matumizi ya mitandao duniani hauonyeshi dalili yoyote ya kupungua huku maelfu ya watu wakiingia mtandaoni kila siku. Ukuaji huo ndiyo unaochochea matumizi ya mitandao ya kijamii.

Ripoti hiyo iliyojikita kuangalia mwenendo wa matumizi ya mitandao ya kijamii hasa Januari mwaka huu, inaeleza kuwa watu bilioni 3.5 duniani ambapo ni sawa na kusema asilimia 45 ya idadi ya watu wote duniani wanatumia mitandao ya kijamii. Na kundi la vijana ndiyo vinara wa mitandao ya kijamii. 

Takwimu hizo zinaashiria kuwa dunia inazidi kujikita zaidi katika teknolojia, jambo linalotoa ujumbe hasa kwa vijana wa Tanzania kutafuta namna ya kufaidika na fursa hizo ili kuondokana na changamoto za ajira na umaskini wa kipato.