Vipaumbele vinne vya bajeti ya Serikali 2020-2021
Miradi na shughuli za kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni mwendelezo wa kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21.
- Baadhi ya vipaumbele hivyo ni pamoja na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda na kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu.
- Uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji nchini Tanzania.
Dar es Salaam. Serikali imesema katika mwaka wa fedha wa 2020/21 itatekeleza maeneo manne ya vipaumbele ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kukuza uchumi wa Taifa na kuboresha maisha ya Watanzania.
Waziri wa fedha na mipango, Dk Philip Mpango amesema maeneo hayo ya miradi na shughuli za kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni mwendelezo wa kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21.
Amesema kipaumbele cha kwanza ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda ambapo serikali itajikita zaidi katika uendelezaji na ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini.
Serikali itafungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuendeleza huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na upatikanaji wa maji sa na salama kwa Watanzania.
“Tutaendelea kusomesha kwa wingi wataalamu kwenye fani na ujuzi adimu kama vile udaktari, mafuta na gesi, Jiolojia, Jemolojia na Uhandisi migodi; kuendelea kugharamia utoaji wa elimumsingi bila ada,” amesema Dk Mpango.
Uboreshaji wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji uiashara na wekezaji ambapo miradi itakayotekelezwa katika eneo hili italenga kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu wezeshi ili kurahisisha uendeshaji biashara na uwekezaji nchini.
“Miradi hiyo ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kimataifa cha standard gauge(kiwango cha kisasa), kuendelea na ukarabati wa vichwa vya treni, mabehewa ya mizigo na abiria pamoja na njia za reli ya kati na TAZARA,” amesema Waziri huyo akianisha kipaumbele cha tatu.
Zinazohusiana:
- Serikali ya Tanzania yaanika vipaumbele vinne bajeti 2019-2020
- Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 5.5 mwaka 2020
Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2020/21 ambapo miradi itakayotekelezwa inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji na usimamizi wa Mpango, kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha za kutekeleza mpango na kuweka vigezo vya upimaji wa matokeo ya utekelezaji.
Amesema miradi hiyo itajumuisha maeneo ya utawala bora hususan utoaji haki na huduma za kisheria, kuimarisha miundombinu ya mahakama, bunge na vyombo vya ulinzi na usalama.
Aidha, Serikali imesema mpango huo utazingatia umuhimu wa kuimarisha Muungano wa Tanzania bara na Zanibar kwa usimamizi wa shughuli za uvuvi, kuboresha programu za mabadiliko ya tabianchi na mpango wa kunusuru kaya maskini.
“Katika mwaka 2020/21, msukumo mkubwa utawekwa katika kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea ili kupata matokeo tarajiwa,” amesema Dk Mpango.