October 6, 2024

Vipimo homa ya dengue sasa kutolewa bure hospitali za umma

Serikali yajipanga kutokomeza maambukizi mapya kwa kuangamiza mazalia na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya.

Mikoa iliyoathirika na ugonjwa huo ni pamoja na Dodoma wagonjwa watatu, Tanga (207), Pwani (57), Morogoro (16) na Singida waligundulika wagonjwa wawili. Mikoa mingine ni Kagera wawili na Arusha watatu. Picha|Mtandao.


  • Vipimo vya ugonjwa huo vitatolewa bure katika vituo vya afya vyote vya umma.
  • Wagonjwa 2,329 wamegunduliwa huku asilimia 93 wakitokea Dar es Salaam.
  • Serikali yajipanga kutokomeza maambukizi mapya kwa kuangamiza mazalia na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya. 

Dar es Salaam. Wakati homa ya dengu ikiendelea kuwatesa Watanzania, Serikali imesema vipimo vya ugonjwa huo vitatolewa bure katika vituo vyote vya afya vya umma.

Hatua hiyo, Serikali inaeleza kuwa itaenda sanjari na upatikanaji mzuri wa dawa katika maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuanzia Januari hadi Juni 19 mwaka huu, watu wanne wamefariki dunia huku wagonjwa 4,320 wameripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini. 

Mkoa wa Dares Salaam unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wanaofikia 4,029 sawa na asilimia 93.06 ya wagonjwa wote walioripotiwa nchini. 

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amelieleza Bunge leo (Juni 21, 2019) kuwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo, Serikali imeamua kutoa bure vipimo  ili kuwapa wananchi ahueni ya matibabu katika vituo vya afya. 

“Serikali imeamua kuwa vipimo kwa ajili ya homa ya dengue vitatolewa bure kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma wakati huu wa mlipuko,” amesema Ummy.

Amesema sambamba na hilo, watahakikisha dawa muhimu za kutibu ugonjwa huo zinapatikana katika vituo vya afya na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya kutoa huduma bora na kuutokomeza ugonjwa huo. 

“Kuimarisha uchunguzi wa homa ya dengue ambapo Bohari ya Dawa (MSD) imeshanunua vipimo 30,000 vya kupima homa ya dengue. Awali Wizara iliagiza vituo vya afya vya umma kutoa huduma za vipimo vya dengue kwa utaratibu wa kawaida wa uchangiaji wa gharama za matibabu,” amesema Waziri huyo. 

Kabla ya Serikali kuweka utaratibu mpya wa vipimo bure, kulikuwa na malalamiko ya wananchi kuwa gharama za matibabu ya ugonjwa huo ziko juu na baadhi yao kushindwa kumudu hasa katika vituo vya afya vya binafsi.


Zinahusiana:


Wakati Serikali ikiendelea kidhibiti ugonjwa huo na maambukizi mapya, itakuwa na kibarua kigumu cha kutoa elimu kwa wananchi juu ya usafi wa mazingira na  kuwawezesha wahudumu wa afya kufuata kikamilifu miongozo ya matibabu ya ugonjwa wa homa ya dengue. 

“Kumekuwa na changamoto ya kudhibiti mlipuko wa homa ya dengue nchini. Changamoto hizi ni pamoja na jamii bado haijaweza kushiriki kikamilifu katika kampeni ya usafi wa mazingira ambayo ndiyo njia kuu ya kudhibiti mazalia ya mbu,” amesema.

Kutokana na juhudi za Serikali na wadau wa afya kupambana na ugonjwa huo, maambukizi mapya kwa mujibu wa Wizara ya Afya yamepungua kutoka wagonjwa 2,294 Mei, 2019 hadi wagonjwa 813 kufikia Juni 19 mwaka huu.

Mikoa iliyoathirika na ugonjwa huo ni pamoja na Dodoma wagonjwa watatu, Tanga (207), Pwani (57), Morogoro (16) na Singida waligundulika wagonjwa wawili. Mikoa mingine ni Kagera wawili na Arusha watatu.