Vita dhidi ya habari za uzushi yazidi kupamba moto Tanzania
Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa imeandaa programu maalum ya uthibitishaji taarifa (Fact checking) ambayo itaisaidia jamii kukabiliana na taarifa za uzushi kuhusu CIVID-19 ikiwa ni safari ya kuwa kurasa maalum za kuthibitisha habari kwenye t
- Nukta Habari yaanzisha programu maalum ya kubaini habari za uzushi na kutafuta ukweli kuhusu taarifa kuhusu Corona.
- Programu hiyo inalenga kuilinda jamii na habari za uzushi na kuchangia kutokomeza janga la COVID-19.
Dar es Salaam. Wakati ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) ukiendelea kuitesa dunia, viongozi na wananchi wanakabiliwa na changamoto nyingine ya kusambaa kwa habari za uzushi na upotoshaji kuhusu ugonjwa huo ambazo zimekuwa na athari kubwa kuliko janga lenyewe.
Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa imeandaa programu maalum ya uthibitishaji taarifa (Fact checking) ambayo itaisaidia jamii kukabiliana na taarifa za uzushi kuhusu CIVID-19 ikiwa ni safari ya kuwa kurasa maalum za kuthibitisha habari kwenye tovuti na mitandao ya kijamii.
Programu hiyo itakayowezeshwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Internews Tanzania imelenga kutumia zana za kidijitali kubaini, kufuatilia na kuzitafutia ukweli taarifa zenye mashaka zinazowekwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp na Facebook.
Licha ya kutumia zana za kidijitali kuzithibitisha habari pia zitakuwa zinatafutiwa ukweli kutoka vyanzo vya uhakika vya mamlaka za afya kama Wizara ya Afya na (WHO) ambavyo vimepewa jukumu la kutoa taarifa rasmi na ushauri kuhusu masuala ya COVID-19.
Habari hizo zitaanza kuchapishwa leo katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya Facebook, Twitter na Instagram kupitia @NuktaFakti ambazo zinamilikiwa na tovuti ya Nukta Habari.
Tovuti ya Nukta Habari ni sehemu ya familia ya Nukta Africa.
Huduma hiyo maalum ya habari si tu itahusika kuthibitisha taarifa za Corona bali itajikita katika kuandaa habari za takwimu zilizochambuliwa vizuri kuhusu halisi ya maambukizi ya Corona katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, Afrika Mashariki na duniani kwa jumla.
Itakuwa ni fursa kwa watu kupata dondoo muhimu ya kuongeza uelewa wa janga hilo kwa kutumia njia rahisi na inayoeleweka haraka ya infografia (Infographics) kufikisha ujumbe wa jinsi ya kujikinga ambazo zitakuwa zinatengenezwa kila wiki.
Soma zaidi:
- Nukta Africa yateuliwa katika mpango wa Google
- Internews, Nukta Africa wafungua fursa ya mafunzo kwa wanahabari Tanzania
Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema uthibitishaji wa taarifa kwa sasa siyo jambo la kuachiwa vyombo vya habari na wanahabari pekee kutokana na kasi ya kusambaa kwa habari za uzushi kipindi hiki cha mlipuko wa COVID-19.
“Pamoja na kwamba tumekuwa tukitafuta ukweli wa habari mbalimbali za uzushi kwa miaka miwili sasa, Nukta Africa kupitia chombo cha habari cha Nukta Habari tumeamua kuanzisha kurasa hizi rasmi za kwenye mitandao ya kijamii ili kuisaidia jamii kupata ukweli wa habari za uzushi zinazosambaa mitandaoni,” amesema Dausen.
Aidha, amesema timu yake itajitahidi kuhakikisha kuwa habari za uzushi zinathibitishwa kama ni ukweli ama la lakini pia kwa msaada mkubwa wa wasomaji wa tovuti ya Nukta ambao wanaombwa kutuma habari ambazo wana wasiwasi nazo kuwa ni uzushi.
Amesema habari za uzushi si za kupuuza kutokana na madhara yake kwa jamii.
Program hiyo inafadhiliwa na mradi wa Boresha Habari unaowezeshwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID). Boresha Habari inasimamiwa na Internews.
Wadau wa karibu katika vita hiyo ya kutokomeza habari za uzushi Tanzania wanasema programu hiyo ni muhimu katika kuimarisha mifumo ya upashanaji habari nchini kwa sababu inakusudia kuwasaidia watu kupata taarifa za kweli.
“Programu hii siyo tu itawasaidia wananchi kukabiliana na habari za uzushi bali hata vyombo vya habari kuwa makini kuzingatia miiko yao katika habari wanazotoa kwa watu ziwe zenye manufaa na zilizohakikiwa,” Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Internews Tanzania, Wenceslaus Mushi ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz).
Amesema, programu hiyo ambayo ni jumuishi, itasaidia katika kupambana na kutokomeza COVID-19 kwa sababu watu wataweza kufanya maamuzi sahihi yanayotokana na taarifa sahihi wanazopata.
Habari hizo zote zitakuwa zinakufikia katika viganja vya mikono kupitia tovuti ya habari ya Nukta (www.nukta.co.tz) na mitandao ya kijamii ya Faceook, Twitter na Instagram ambayo imekuwa ikitumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu ya kutumia COVID-19 kuathiri maisha ya watu na shughuli zao.
Ni muhimu kufahamu kuwa programu hii ni endelevu na haitahusika tu katika uthibitishaji wa taarifa za uzushi kuhusu Corona bali itajenga msingi kwa Nukta kuwalinda wasomaji wake na wananchi dhidi ya taarifa za uzushi.