Viti maalum vinavyoweza kuokoa maisha watoto kwenye magari binafsi
Wadau wapendekeza marekebisho ya sheria ya Usalama barabarani kuwalazimisha wazazi kununua vizuizi vya watoto
- Tumia kizuizi cha mtoto kumlinda mwanao katika gari lako.
- Wadau wa marekebisho ya sheria ya Usalama barabarani.
Dar es Salaam. Wakati unaendesha gari huku mtoto wako akiwa amekaa pembeni umewahi kufikiri madhara yanayoweza kumpata pindi gari litakaposimama ghafla au likipata ajali.
Madhara hayo ni pamoja na magonjwa ya akili, ulemavu hata kifo. Kimsingi watoto wadogo hawawezi kujisimamia wenyewe na wanahitaji msaada wa mzazi au mlezi kuhakikisha wakati wote wanakuwa salama.
Kama mtu mzima anatakiwa kufunga mkanda wakati wote akiwa kwenye gari, ni zaidi kwa mtoto ambaye hawezi kuhimili mitikisiko au jambo lolote baya linaloweza kutokea kwenye gari.
Wakati watu wazima wakifunga mikanda, watoto wadogo wanatakiwa kutumia vifaa maalum ambavyo hujulikana zaidi kama vizuizi vya watoto hasa katika magari binafsi.
Vizuizi vya watoto ni viti maalum vyenye mikanda mahususi kumlinda mtoto ambapo vimetengenezwa kulingana na uzito, urefu na umri wa mtoto.
Licha ya umuhimu wa kuwa na viti maalum vya watoto kwenye magari, Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 haijaweka wazi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kumlinda mtoto dhidi ya hatari yoyote inayoweza kutokea kwenye gari.
Kwa mujibu wa ripiti ya Shirika la Afya duniani (WHO) kuhusu hali ya usalama barabarani ya mwaka 2015 inaeleza kuwa ni nchi 53 pekee duniani zina sheria ya matumizi ya vizuizi vya watoto ambapo Tanzania haipo kwenye nchi hizo na kubainisha ni wazazi wachache wenye uelewa wa matumizi ya viti hivyo na jinsi ya kumlinda mtoto kwenye gari.
WHO inaeleza kuwa watoto wachanga hadi wenye miaka 11 wanapaswa kutengewa kiti maalum kinachoweza kumtosha kulingana na uzito, umbo lake akiwa kwenye gari binafsi.
“Mimi mwaka jana (2017) nilipata ajali na ‘Airbag’ (Mfuko maalum wa kumkinga mtu asiumie kwenye ajali) haukufanya kazi niliumia sana, sasa fikiria kama mtoto umempakata kiti cha mbele alafu akapata ajali! Wazazi ni wakati wa kutumia viti hivyo na kuhakikisha hawakai siti za mbele,” anasema Neema Komba mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam.
Ili kuhakikisha zaidi usalama wa mtoto, viti hivyo maalum vinapaswa kufungwa kwenye siti za nyuma na wadau wa usalama barabarani hawashauri mtoto kukaa siti za mbele ili kuepuka kuchomoka kwa mtoto pindi ajali inapotokea au gari linaposimama ghafla.
Kizuizi cha mtoto kilichofungwa kwenye siti ya nyuma ya gari kikiwa na mikanda maalum. Picha| Vicensia Fuko
Wakati wazazi wanawaza kununua magari ya kifahari, wanashauriwa pia kufikiria jinsi ya kuwalinda watoto wao kwa kuwanunuliwa vizuizi ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kuzuilika.
“Nimekinunua vizuizi vya watoto kwasababu za kiusalama tu, mikanda ya gari haitoshi kwa ajili ya usalama wa mtoto mdogo,” anasema Khamis Shekibula mkazi wa Kinyerezi ambaye amemnunulia mtoto wake mdogo, “Gharama zake sio kubwa sana, mimi nilinunua cha sh 300,000 ila vipo chini ya hapo inategemea unachokitaka.”
Vizuizi vya watoto vinapatikana katika maduka mbalimbali yanayojihusisha na uuzaji wa vifaa na nguo za watoto. kwa Dar es Salaam vinapatikana kwenye maduka ya Babyshop, Toto Junction, Game ambapo huuzwa kati ya Sh150,000 na 450000 kutegemeana aina na ukubwa.
Mabadailiko ya sheria
Wadau mbalimbali wanaishauri Serikali kuongeza mkazo wa kuwalinda watoto pamoja na kuifanyia mabadiliko sheria ya Usalama Barabarani ili wazazi wawajibike kuwanunulia watoto wao viti maalum.
“Mzazi asisubiri hadi sheria imbane anunue kizuizi cha mtoto kwenye gari, wanaopata madhara ni watoto wao wenyewe,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Jones John.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama barabarani Tanzania (Road Safety Ambassadors RSA), John Seka ameiambia nukta kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi ya vizuizi vya watoto na mabadiliko ya sheria.
“Tunategemea kabla ya mwaka 2018 haujaisha basi muswada wa marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, ufikishwe bungeni na vizuizi vya watoto kuwa lazima katika magari binafsi ili kuweza kumlinda mtoto kwani ni haki yake kulindwa na madhara yoyote,” anasema John.
Watoto wakiwa katika viti vyao maalumu ambavyo vinawalinda na kuwafanya wawe salama zaidi wakiwa barabarani.Picha| Queen Paul
Kwanini vizuizi vya watoto ni muhimu
WHO inafafanua kuwa robo tatu (73%) ya ajali zote za barabarani zinawapata vijana wa kiume walio chini ya umri wa miaka 25 ambao wana uwezekano wa kufa mara tatu zaidi kwenye ajali hizo zaidi ya wasichana.
Mwaka 2004, ajali za barabarani zilisababisha vifo 260,000 kwa watoto na vijana walio na umri kuanzia 0 hadi 19 (0-19). Vifo vya watoto ni asilimia 21 ya ajali zote za barabarani duniani ambapo ajali hizo hutokea zaidi katika nchi za Kusini Mashariki mwa Asia na Afrika.