October 7, 2024

Vodacom yafungua fursa za kiuchumi wilayani Mpanda

Imezindua duka la kisasa katika wilaya hiyo litakalowaunganisha wananchi na fursa za kiuchumi na kijamii hasa katika sekta ya mawasilino.

Kwa sasa Vodacom Tanzania Plc ina maduka 100, madawati ya huduma kwa mteja (Service Desks) 350 yanayotoa huduma kwa wateja wa kampuni hiyo maeneo mbalimbali nchini. Picha| Mtandao.


  • Imezindua  duka la kisasa katika wilaya hiyo litakalowaunganisha wananchi na fursa za kiuchumi na kijamii hasa katika sekta ya mawasilino.
  • Lina wafanyakazi 15 na vifaa vya kisasa kutoa huduma bora ikiwemo jukwaa la mtandaoni la kuhifadhi pesa la M-Koba. 
  • Waziri Mkuu mstaafu Pinda awataka wananchi kuchangamkia fursa ili kukuza uchumi wa wilaya hiyo. 

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha inasogeza huduma karibu na wateja na kuongeza ushindani katika sekta ya mawasiliano nchini, kampuni Vodacom Tanzania imezindua duka la kisasa katika wilaya ya Mpanda mkoani Katavi litakalowafungulia fursa mbalimbali za kijamii na kiuchumi wananchi wa wilaya hiyo na maeneo yanayoizunguka.

Huduma zinazotolewa katika duka hilo ni pamoja na usajili wa laini za simu, ushauri wa huduma za Vodacom kama M-Koba, kurudisha laini zilizopotea au kuharibika na kununua simu janja kwa bei nafuu. 

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa duka hilo jana (Aprili 23, 2019) amesema duka hilo litarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja na kuchochea shughuli za kiuchumi za wilaya na mkoa huo.

“Karibuni nyumbani Vodacom, hongereni sana kwa kutufungulia duka kubwa zaidi hapa Mpanda kwani wilaya hii ina wananchi wachapakazi, wenye muamko wa kukuza uchumi na wafanyabiashara wakubwa na wadogo,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo, Pinda amesema ni furaha kuona wananchi wanapata huduma za simu kwa ukaribu huku wajasiriamali na wakifaidika na fursa mbambali ikiwemo M-Koba ambapo amewahamasisha wakazi wa wilaya hiyo kuona duka hilo kama kichocheo cha kukuza uchumi wilayani humo.

Duka hilo na madawati ya huduma kwa mteja lililoajiri wafanyakazi 15 lina vifaa vya kisasa, wafanyakazi waliopata mafunzo ya kutoa huduma bora kwa wakazi wa wilaya ya Mpanda kwa kuzingatia ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Katavi.


Soma zaidi:


Naye Mkuu wa mauzo wa Vodacom Kanda ya Nyanda za Juu kusini, MacFydine Minja amesema uzinduzi wa duka hilo unaenda sambamba na mkakati wa kampuni hiyo wa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuleta fursa kwa watanzania. 

Pia Vodacom yenye wateja wa simu za mkononi zaidi ya 14 milioni imelenga kupanua wigo wa huduma za simu Tanzania na kuzifikisha karibu na wananchi. 

“Tumejidhatiti kutoa huduma bora kwa wateja wetu katika mkoa huu, ambapo tayari tuna huduma ya 4G ambayo inatoa nafasi ya kupata intaneti yenye kasi zaidi, pia tuna madawati matano ya huduma kwa wateja,” amesema Minja.

Huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi imekuwa ikiongezeka kwa kasi nchini na kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla. 

“Nimekuwa nikipanga kuwa wakala wa M-Pesa kwa muda mrefu sana na sasa naishukuru Vodacom kwa kutufungulia duka hili, kwani leo naanza hatua ya kwanza ya kutimiza ndoto yangu” amesema Helena Lao, mkazi wa wilaya hiyo.

Kwa sasa Vodacom Tanzania Plc ina maduka 100, madawati ya huduma kwa mteja (Service Desks) 350 yanayotoa huduma kwa wateja wa kampuni hiyo maeneo mbalimbali nchini.