October 6, 2024

Vodacom yawekeza Sh11 bilioni huduma za jamii Tanzania

Uwekezaji huo umefanyika kupitia taasisi yake ya Vodacom Tanzania Foundation kati ya mwaka 2014 na 2017 katika sekta za kilimo, afya na elimu.

  • Uwekezaji huo umefanyika kupitia taasisi yake ya Vodacom Tanzania Foundation kati ya mwaka 2014 na 2017. 
  • Wanakusudia kuwekeza tena Sh1 bilioni kila mwaka kwenye elimu na mazingira.
  • Wamejikita zaidi kuinua maisha ya watoto na wanawake kupitia sekta za afya, elimu na kilimo.
  • Serikali yasema itaendelea kushirikiana nao kwa kuwawekea mazingira mazuri ya biashara. 

Dar es Salaam. Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania imesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita iliwekeza Sh11 bilioni katika sekta mbalimbali ikiwemo afya zilizogusa na kuboresha maisha ya wananchi wenye uhitaji katika jamii. 

Kampuni hiyo inayosimamia taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imesema katika kipindi cha mwaka 2019 na 2021 inakusudia kuwekeza Sh1 bilioni kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hasa wanawake na watoto wa hali ya chini. 

Mkurugenzi wa  taasisi hiyo, Rosalynn Mworia  amesema kiasi hicho cha Sh11 bilioni kilitolewa kati ya mwaka 2014 na 2017 ikiwa ni jitihada za mfuko huo kuisaidia jamii yenye uhitaji. 

Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya matokeo ya Vodacom kwa jamii (Social Impact Report and new strategy to deliver inclusive growth) leo Juni 27, 2019, Jijini Dar es Salaam, amesema kupitia sekta za elimu, afya na kilimo wamefanikiwa kuboresha maisha ya watu zaidi ya milioni tatu. 

“Hadi kufikia hapa tumeshawekeza Sh11 bilioni ambazo zimetuwezesha kuwafikia watoto wa kike na wanawake katika kuwasaidia kwenye afya pamoja na uchumi,” amesema Mworia.

Aidha, Mworia amesema mwaka 2019 hadi 2021  watawekeza zaidi katika elimu, uchumi na shughuli ambazo zitasaidia kutunza mazingira ambapo kila mwaka watatoa Sh1 bilioni. 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Joseph Kandege, akikata utepe kuzindua Ripoti ya Jamii  kutoka Vodacom leo Jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliana Tanzania (TCRA), Dk Jones Kilimbe, kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia na Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Hashim Hendi. Picha|Maelezo.

Takwimu za mwaka 2018 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha Vodacom inaongoza kwa kuwa na wateja milioni 14.14 kati ya kampuni za simu saba zinazotoa huduma hiyo hapa nchini. 

Pia inaongoza pia kwa idadi ya wateja wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi kwa kuwa na asilimia 38.6 ya soko ikifuatiwa na kampuni za Tigo (Tigo Pesa) na Airtel (Airtel Money).


Soma zaidi:


 Akizungumza  katika hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo, Naibu  Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Joseph Kandege amesema Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni za simu ikiwemo Vodacom ili kuwasaidia wananchi katika mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo ya afya, elimu  na miundombinu.

“Serikali itaimarisha miundombinu ili kuhakikisha Vodacom inawafikia  watu wenye uhitaji na pia tumeona jinsi walivyoweza kuwasaidia watoto wa kike na wakina mama wenye fistula kupata matibabu  ya ugonjwa huo na kugawa taulo kwa watoto wa kike wenye uhitaji, ambao wanakosa kwenda shuleni pindi wawapo kwenye hedhi,” amesema Kandege.

Amesema matarajio yake ni kuwa  kazi inayofanywa na vodacom  inaweza kufanywa na mashirika mengine kwa kushirikiana na kampuni hiyo ili kuifikia jamii kwa upana zaidi.