October 6, 2024

Vyeti vya uasili kuwapunguzia mzigo wa kodi wajasiriamali Tanzania

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika kuhakikisha sekta isiyo rasmi inaimarika, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara kwa wajasiriamali wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwapatia vyeti vya uasili amb

  • Wajasiriamali hao wanapatiwa vyeti vya uasili ambavyo vimetoa unafuu mkubwa wa kodi na tozo.
  • Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kutoa elimu ili kuwafungulia fursa mbalimbali. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika kuhakikisha sekta isiyo rasmi inaimarika, Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara kwa wajasiriamali wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwapatia vyeti vya uasili ambavyo vimetoa unafuu mkubwa wa kodi na tozo.

Majaliwa alikuwa akizungumza Novemba 24, 2019 wakati akifunga Maonyesho ya Wajasiriamali wa Tanzania kusherehekea miaka 20 ya uanzishwaji wa EAC yaliyofanyika Fumba, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinatambua mchango wa sekta isiyo rasmi, hivyo zimekuwa zikifanya juhudi mbalimbali kuendeleza na kuongeza tija katika sekta hiyo. 

“Vilevile, tuendeleze ujirani mwema, kupanua na kuimarisha ushirikiano wa watu wa Afrika Mashariki ili kuharakisha ukuaji wa kiuchumi sanjari na kuboresha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki kiuchumi, kisiasa na kijamii,” amesema Majaliwa.

Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha wajasiriamali wanachangamkia fursa za kibiashara zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

“Mkakati huo unahusisha zoezi la kufanya utafiti wa uelewa wa Watanzania kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na matokeo ya utafiti huo yatatumika katika kutoa elimu kwa umma kulingana na mahitaji,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.


Zinazohusina: 


Katika kutatua changamoto ya mitaji kwa wajasiriamali, Majaliwa amesema Serikali inatekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 ya kuweka mfumo wa kuvitambua, kuvisajili na kuviwezesha vikundi vyenye mwelekeo wa ushirika na ujasiriamali. 

Amesema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa ni kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa taasisi za fedha na mifuko mbalimbali ya umma na binafsi kutoa mikopo kwa wajasiliamali kwa riba nafuu na ikiwezekana isiyo na riba.

“Katika kipindi cha Julai, 2018 hadi Juni, 2019 mikopo yenye thamani ya Sh42.06 bilioni 42 kwa vikundi 11,487 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ilitolewa. 

“Vilevile, mikopo hiyo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri imeendelea kuzingatia uwiano wa asilimia nne kwa vikundi vya wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu,” amesema Majaliwa. 

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inahamasisha uundwaji wa vikundi vya wajasiriamali, kusimamia utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi hivyo sambamba na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuwezesha wajasiriamali na wawekezaji wengine kufanya shughuli zao bila bughudha.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi ya gazeti, kutoka kwa Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar, Yussuf Khamis, wakati akitembelea mabanda, kwenye Maonesho ya Wajasiriamali, katika Kusherehekea Miaka 20 ya Uanzishwaji Jumuiya ya Afrika Mashariki, yaliyofungwa rasmi Novemba 24, 2019. Kutoka kushoto ni Maafisa Biashara na Matangazo, Rahma Juma,Khalid Hussein na Khadija Khamis. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.

Maonyesho hayo yametoa fursa kwa wajasiriamali kupata ujuzi, taarifa za masoko, teknolojia, mbinu na taratibu mbalimbali za kufanya biashara ili kukuza shughuli zao. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzungumzia kuhusu vikwazo visivyo vya kiforodha vinavyozorotesha wajasiriamali kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo amesema vimeendelea kutatuliwa kupitia majadiliano baina ya Tanzania na nchi nyingine ndani ya Jumuiya hiyo kwa lengo la kuvipunguza na kuviondoa kabisa.

Waziri Mkuu amesema  kupitia majadiliano hayo, Serikali imefanikiwa kuratibu zoezi la uondoaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kiforodha 15 kati ya 24 vilivyoripotiwa mwaka 2019 na vikwazo tisa vilivyobakia hatua ya kuvipatia ufumbuzi inaendelea.