October 6, 2024

Wabunge wazituhumu halmashauri kutoza kodi zilizofutwa na Serikali

Wamesema zipo baadhi ya halmashauri zinazotoza kodi za kero zilizofutwa na Serikali mwaka 2017.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara. Picha|Mtandao.


  • Wamesema zipo baadhi ya halmashauri zinazotoza kodi za kero zilizofutwa na Serikali mwaka 2017.
  • Serikali yasema zikibainika haitasita kuchukua hatua za kisheria
  • Utoaji vitambulisha kwa wajasiriamali kuwekewa utaratibu mpya Julai 1. 

Dar es Salaam. Kufuatia kuwepo kwa madai ya baadhi ya Halmashauri kuwatoza wananchi kodi zilizofutwa na Serikali, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara amesema Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa halmashauri yoyote inayoendelea kutoza kodi hizo.

Mbali na hatua hiyo, Julai 1 mwaka huu Serikali imesema itatoa waraka utakaoanisha watu wanaopaswa kupata vitambulisho vya ujasiriamali ili kuondoa mkanganyiko wa utekelezaji wa zoezi hilo katika halmashauri. 

Ametoa ufanunuzi huo Bungeni leo (Juni 25, 2019) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kavuu, Dk Pudenciana Kikwemba aliyetaka kujua ni kwanini baadhi ya halmashauri zinakaidi agizo la Rais John Magufuli la kukemea utozaji wa kodi ambazo zimekuwa kero kwa wananchi. 

Akijibu swali hilo, Waitara amesema kodi za kero zilifutwa na Serikali kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa sura na 290 mwaka 2017 na halmashauri yoyote inayoendelea kuwatoza wananchi kodi ambazo zilifutwa kwa mujibu wa sheria inakiuka maagizo ya Serikali. 

“Natoa fursa hiii kuziagiza halmashauri kuacha kutoza kodi ambazo zimefutwa kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Tamisemi haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa halmashauri ambayo itabainika kuwatoza wananchi kodi ambazo zimefutwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Waitara. 

Aidha, amesema kama Mbunge Dk Kikwemba anazo taarifa za halmashauri zinazotoza kodi ambazo zimefutwa aipatie ofisi yake ili ichukue hatua. 

Baada ya majibu hayo, alisimama Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na kuishauri Tamisemi kuangalia uwezekano wa kutoa waraka kwa halmashauri zote ikiainisha kodi zote zilizofutwa na Serikali ili kuondoa usumbufu unaojitokeza sasa.


Zinazohusiana:


Akizungumzia suala hilo, Waitara amesema wamepokea ushauri huo na ameahidi  kuwa waraka huo utatengenezwa na utasambazwa nchi nzima ili kuonyesha kodi za kero zilizofutwa. 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amesema ifikapo Julai 1 mwaka huu, Serikali itatoa waraka unaoainisha watu wanaopaswa kupewa vitambulisho vya wajasiriamali ili kuepusha usumbufu unaojitokeza katika utekelezaji wa agizo hilo la Rais Magufuli. 

Amesema baada ya waraka huo kutolewa, halmashauri au watu watakaokiuka masharti yake watachukuliwa hatua kali za kisheria. 

Ufanunuzi huo umetolewa baada ya Chenge kuhoji kuwa Serikali haioni haja ya kuwa na utaratibu unaofanana nchi nzima wa utoaji wa vitambulisho hivyo, kuliko hivi sasa ambapo imekuwa kero kubwa.