Wabuni huduma za ofisi kuwawezesha wajasiriamali wanawake Dar
Wajasiriamali hao wanaweza kukodi ofisi kwa muda wanaotaka kutumia na kupata mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali.
- Ni wakati wa wanawake wajasiriamali kukutana na kufahamiana.
- Wajasiriamali wanawake watoa maoni yao wakisema baadhi ya wanawake watashindwa kumudu gharama hizo.
Namna eneo la ofisi inayotumiwa na watu wengi inavyokuwa ili kuwawezesha kuweza kushirikiana pamoja. Picha| www.musique-jazz.com
Dar es Salaam. Kutokuwa na eneo maalum la kufanyia biashara hasa kwa kampuni mbalimbali zinazochipukia katika ulimwengu wa biashara au mtu anayefanya kazi za kujiajiri mwenyewe ni moja ya changamoto kwa waanzilishi wengi.
Hivyo watu au kampuni mbalimbali huchukua fursa ya kuwapangisha wafanyabiashara au wajasiriamali katika ofisi mbalimbali kwa malipo maalum wanayokubaliana, ila sehemu nyingi jukumu lao kubwa ni kukukodisha eneo la ofisi tu, lakini wengine wanaenda mbali zaidi.
Kampuni ya Safe Space iliyopo Masaki, Dar es Salaam yenyewe imeamua kuwekeza katika kutoa huduma ya ofisi inayohusisha ukumbi wa kufanyia vikao, huduma ya kifungua kinywa, sehemu ya ofisi yenye mtandao wa intaneti, mafunzo na mbinu mbalimbali za kukuza masoko kwa wanawake.
Mbali na huduma hizo zinazotolewa kama kifurushi, Safe Space kukutanisha wanawake wajasiriamali, waliojiajiri wenyewe au wanaofanya kazi za utafiti kufanya shughuli zao katika eneo moja.
“Tunawajengea wanawake uwezo kwa kuwaunganisha katika sehemu moja ili waweze kufahamiana kwa vitu wanavyofanya,” amesema Meneja wa Maudhui na Jamii, Selam Ahmed.
Hata hivyo, ili mtu aweze kupata nafasi inabidi alipie kwa mwezi kutokana na uwezo wake na alivyojipanga kufanya kazi zake.
“Tuna malipo ya aina mbili, kwa wanaokuja siku tano kwa wiki kwa mwezi atalipia Dola za Marekani 150 sawa na Sh350,400 na kwa wanaokuja siku tatu kwa wiki kwa mwezi atalipia dola 60 sawa na Sh136,200” ameeleza Ahmed.
Baadhi ya wajasiriamali wamesema kuanzishwa kwa huduma hiyo ni jambo la kiubunifu na litawasaidia wanawake katika kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda lakini wakapaza sauti kuwa bei ya sasa ni kubwa inayoweza kuwatenga wale wasio na uwezo.
“Inategemea na bidhaa unayouza kwa jinsi eneo la ofisi lilipo wateja wangu wengi hawawezi kufika huko,” amesema Royda Mwakamele, mjasiriamali wa nguo za mtumba mtandaoni.
Ila kwa Mariam Ibrahim ambaye ni mwanzilishi wa Kampuni ya Najj Food Processing ameiona hiyo ni fursa kwake kama mjasiriamali kupata nafasi ya kukutana na wanawake wengine na kuonyesha biashara yako kwa wengine.
Mariam anasema gharama za kulipia kwa wajasiliamali wadogo ambao ndio kwanza wanaanza biashara ukiachana na wale ambao wameshakuwa na jina tayari.
Zinazohusiana: Mambo ya kuzingatia unapoanzisha brand yako ya biashara
Acha kuwaza kuwa mfanyabiashara, anza kufanya biashara
“Bei ni kubwa kwa mjasiriamali anayeanza na kuna uhaba wa masoko, licha ya kwamba wanaweza kukufundisha mbinu za kupata masoko,” amesema Mariam.
Rebeca Gyumi, Mwanzilishi wa Msichana Initiative kupitia mtandao wake wa Instagram anawataka wajasiriamali kuanza mdogomdogo ili mradi wanapiga hatua.
“Tulikodi seat (siti) moja mwanzoni, tunapokezana kwenda ofisini, baadae tukaongeza viti viwili, Mungu jalia tunaofisi yetu sasa” anasema Gyumi.
Hata hivyo, katika kuelekea katika kumnyanyua mwanamke katika sekta ya uchumi, maeneo kama Safe Space yakitumiwa vizuri itakuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa mwanamke mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla lakini yanapaswa kuendana na hali halisi ya uchumi wa wanaolengwa kuyatumia.