July 8, 2024

Wabuni teknolojia ya kurahisisha upatikanaji wa taarifa za elimu Tanzania

Elimu Yangu imelenga kuwasaidia wanafunzi, wazazi na walezi kujua ufaulu wa shule husika zikiwemo zile zilizopo kwenye 10 bora na mkiani.

  • Elimu Yangu inawasaidia wanafunzi, wazazi na walezi kujua ufaulu wa shule husika zikiwemo zile zilizopo kwenye 10 bora na mkiani.
  • Wahitimu wa kidato cha sita pia wanaweza kubaini iwapo alama zao zinawaruhusu kusoma kozi fulani chuo kikuu ama la.
  • Programu hiyo imelenga kuwafikia watu wengi zaidi ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu elimu nchini.

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu wazazi wengi na walezi wamekuwa wakihaha kupata taarifa za kina juu ya shule wanazosoma watoto wao hasa katika ufaulu. Mbali ya kujua iwapo watoto wao wamefaulu ama la, kwa baadhi imekuwa vigumu kujua ufaulu wa shule husika. Wapo ambao watoto wao husoma shule bora na wengine za wastani au zinazofanya vibaya.

Licha ya kuwepo taarifa mbalimbali za matokeo ya mitihani katika tovuti ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta),siyo wote wanaweza kuchambua kujua orodha ya 10 bora au zile za mwisho kwa shule za sekondari kitaifa, kimkoa na hata kiwilaya ikitokea. Mara nyingi nyingi shule zinazofahamika zaidi ni zile 10 bora au zile zilizofanya vibaya kitaifa. 

Hata hivyo, kama wewe ni miongoni mwa wazazi, walezi au wanahabari ambao walikuwa wanahitaji taarifa za kina kuhusu ufaulu wa shule mbalimbali nchini basi usiwaze. Teknolojia inazidi kurahisisha zaidi upatikanaji wa taarifa hizo za ufaulu kwa kuchambua takwimu za matokeo katika lugha rahisi.

Miongoni mwaprogramu za kiteknolojia zinazotoa huduma hizo ni Elimu Yangu iliyoanzishwa hivi karibuni ikiwa imejikita kutoa taarifa za elimu kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.

Tovuti  ya Elimu Yangu iliyoanzishwa na taasisi ya Code for Africa na Code for Tanzania imejikita kutatua matatizo ya upatikanaji taarifa muhimu kuhusu shule na elimu ya juu.

Hadi sasa kupitia Elimu Yangu wanafunzi  wanaweza kuchagua shule wanayoipenda kuanzia ngazi ya Sekondari na itakayoendana na kile atakachokisomea hapo baadaye katika ngazi ya chuo kikuu. 

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari hususan kidato cha sita tovuti hiyo inaweza kuwapa majibu iwapo alama walizopata zinafaa kusomea kozi wanazopenda ama la kwa kutumia sifa na vigezo vilivyowekwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).

Mmoja wa waliohusika kuandaa tovuti hiyo kutoka Code for Africa, Taha Jiwaj anasema lengo jingine ni kuwasaidia wazazikujua shule ipi nzuri kwa mtoto wake na pia kubashiri malengo ya baadaye ya wanawe. Kupitia Elimu Yangu mwanafunzi anaweza kujua alama anazotakiwa kuwa nazo ili siku za mbeleni awe mhandisi au daktari kwa vigezo vya TCU. 

Sambamba na hilo tovuti au programu hiyo inaweza kutumika na  wanahabari au watafiti kwa ajili ya kuwasaidia kuandika habari za takwimu  zilizochambuliwa kwa kina. Wanaweza kupata ramani, grafu na takwimu katika lugha rahisi.

Taha anasema takwimu zilizopo nyuma ya mfumo huo ni matokeo ya mitihani ya Necta ambayo hutolewa kila mwaka na kuziweka katika tovuti yao

Hata hivyo, ili wasomaji wazielewe kirahisi takwimu, anasema  hivyo takwimu wamelazimika kuzichambua kwa kina na kuziweka katika mfumo wa kompyuta unaojibu maswali ya watumiaji pale wanapotaka kujua jambo kuhusu matokeo ya shule husika za sekondari.

Miongoni mwa huduma maarufu katika mfumo huyo wa Elimu Yangu ni orodha ya shule 10 bora kitaifa, kimkoa na kiwilaya hivyo hivyo kwa shule za mkiani katika ufaulu.

Vile vile mfumo huo utawawezesha watumiaji kujua shule gani ni bora katika masomo ya sayansi au sanaa. Ili kuleta picha ya ushindani kamili katika shule za sekondari kama ambavyo Necta hufanya, wasanifu wa Elimu Yangu wamezipanga shule za sekondari nchini katika makundi ya shule zenye wanafunzi 40 au zaidi na zile zenye wanafunzi chini ya 40. 

Taarifa nyingine muhimu kwa wazazi au walezi katika mfumo huo ni mkoa au wilaya ambako shule hizo zinapatikana ili kumpa mzazi taarifa sahihi zitakazomsaidia kufanya maamuzi kabla ya kumpeleka mtoto wake shule. Pia inaweza kukusaidia kuchagua mchepuo wa kuchukua katika shule za kidato cha tano na sita.

Wazo la elimu yangu lilianzaje

Wazo hilo ni matokeo ya utafiti wa changamoto za kielimu zilizoibuliwa na mradi wa kukuza matumizi ya takwimu nchini wa Data Zetu ambao unafanywa katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Halmashauri ya wilaya ya Kyela na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Ili kuzitatua changamoto hizo zikiwemo uhaba wa taarifa za kina kwa wazazi, wabunifu wa mfumo huo waliona ni vyema kutumia takwimu zilizopo ili kutoa uwanda mpana wa taarifa kwa wananchi kwa kuwa siyo watu wote wana uwezo wa kuzichambua.

Malengo ya baadaye

Mfumo wa Elimu Yangu unategemewa kushuka mpaka chini hadi katika ngazi ya elimu ya msingi hivyo mfumo huu utakuwa wa kipekee kwa kuwa utakuwa na habari za takwimu kuanzia shule za msingi kwa maana ya matokeo y a darasa la saba  mpaka vyuo vikuu.

Baadaye kuna mpango wa kuongezea vyuo pamoja na vyuo vikuu bila kusahau vyuo vya mafunzo ili kutanua wigo kwa mwanafunzi na mzazi kuchagua kwenye elimu.

Malengo mengine ya badaye ni kuongeza mchanganuo wa takwimu wa matokeo kufikia angalau miaka mitano nyuma kuanzia sasa .

Mbali na mikakati hiyo, waanzilishi wa mfumo huo Code for Tanzania wanataka kuwafikia watu wengi zaidi wakishirikiana na vyombo vya habari katika kutumia mfumo huo ili uweze kuwafikia  wananchi wengi zaidi.

Elimu Yangu itawazidi washindani?

Hata wakati Elimu Yangu ikiingia sokoni mwishoni mwa Aprili, bado kuna huduma nyingine za teknolojia  kama Shule Wiki, school.co.tz sambamba na matokeo.co zote zikiwa na malengo ya kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu zitakazokuza sekta ya elimu.

Hata hivyo, tofauti kubwa iliyopo katika huduma hizo na Elimu Yangu ni namna mtumiaji anavyoweza kupata huduma nyingi zinazoendeshwa kwa takwimu yakiwemo matokeo   kidato cha nne mpaka ubashiri wa elimu katika vyuo vikuu kuanzia ngazi ya wilaya mpaka ngazi ya Taifa .

Ubunifu huo wa teknolojia unakuja wakati takwimu mpya za robo ya mwisho wa mwaka 2017 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imepaa kwa asilimia 15 hadi watumiaji milioni 23 mwaka 2017 kutoka milioni 19.86 wa mwaka 2016. Kiwango hicho ni zaidi ya mara tatu ya kile kilichorekodiwa miaka mitano iliyopita.