October 6, 2024

Wabunifu wakumbushwa kuigeukia nishati vijijini

Wabunifu waitwa kutizamia nishati mbadala kama vumbuzi zitakazo saidia wakazi wa vijijini

  • Wametakiwa kubuni teknolojia rahisi zinazotumia nishati jadidifu ili kuwarahisishia maisha wakati wa vijijini katika shughuli za uzalishaji mali
  • Wadau wa teknolojia wazitaka kampuni za teknlojia zinazochipikia kujitokeza ili zisaidiwe kujitanua. 

Dar es Salaam. Mkuu wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe amewataka wabunifu kugeukia maeneo ya vijijini na kutengeneza teknolojia rahisi zinazoweza kusaidia wakazi wa maeneo hayo kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa nishati mbadala.  

Akizungumza na Wanahabari leo (Machi 25, 2019) katika  ufunguzi wa “Wiki Ya Ubunifu” jijini Dar es Salaam, amesema wabunifu wengi wanatatua matatizo ya wakazi wa mjini na wanasahau ya kuwa takriban asilimia 80 ya watanzania wanakaa vijijini na wanahitaji matokeo ya ubunifu wao katika kurahisisha maisha hasa katika shughuli za uzalishaji na kilimo.

“Waingie vijijini waone changamoto ambapo changamoto hizi kwa wabunifu ni fursa kuweza kubuni njia bora za kutatua matatizo ya watanzania ambao asilimia 75 hadi 80 wanaishi vijijini,” amesema  Gondwe.

Amesema ni bora zaidi kama wabunifu hao wataangazia kutengeneza teknolojia zinazotumia nishati asilia kama umemejua kwani zitakuwa msaada hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na nishati ya umeme wa gridi ya taifa.

Mashine zinazoendeshwa kwa umemejua zinasaidia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ukaushaji wa zao la muhogo, kukamulia mafuta.

“Mkulima anaweza kutumia teknolojia rahisi kama sola. Je wamejifungia ndani na kuweza kutengeneza teknolojia rahisi ambayo mkulima kijijini anaweza kutumia jua kutengeneza mashine ya kuchakata muhogo, alizeti?” amehoji Gondwe.


Zinazohusiana: 


Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi amesema kuna haja ya Serikali na wadau wa teknolojia kuangalia namna ya kuwainua wabunifu kufikia malengo yao kwa kuwapatia msaada wanaouhitaji.

Amesema sio kweli kuwa vumbuzi na mawazo ya ubunifu hayapo bali changamoto ni kuweza kuzipata kampuni zinazochipukia na kuzisaidia kukua kwa sababu ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa viwanda.

“Vumbuzi na mawazo ya kibunifu yapo, tunahitaji kufikiria ni kwa jinsi gani tunaweza kuzifahamu kampuni changa na kuzisaidia kukua,” amesema.

Hata hivyo, wabunifu wametakiwa kutengeneza teknolojia rahisi zenye uwezo wa kutumia umeme mdogo ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuwafikia watu wengi. 

Grace Mzee ambaye ni mfuga kuku maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam aliyefanikiwa kuhudhuria ufunguzi huo amesema teknolojia nyingi zinazotengenezwa zinamuongezea mawazo mtumiaji kwani huja na mahitaji mengi.

“unakuta mashine inaletwa, inakula umeme, bado hujanunua chakula cha kuku, bado hujalipia bili ya maji, bado chanjo, huku umewasha taa za njano umeme wote unaisha,”amesema

Grace ambaye anamiliki mashine ya kutotoresha vifaranga ambapo anasema mashine hiyo hutumia umeme mwingi na angeona ahueni kama mashine hiyo ingetumia umemejua.