October 7, 2024

Wachambuzi wa biashara waelezea Jumia kufunga vilago Tanzania

Hatua hiyo ya Jumia inakuja siku chache baada ya kusimamisha oparesheni zake nchini Cameroon kusema inaangazia masoko sehemu nyingine duniani.

  • Wamesema bado Watanzania wanakumbatia mifumo ya asili ya manunuzi
  • Wengine wamesema ukosefu wa elimu ya biashara ya mtandaoni ndiyo sababu.
  • Washauri mamlaka kuongeza uwekezaji wa mifumo ya kisasa ya biashara.

Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya biashara wameelezea hatua ya kampuni inayoendesha soko la mtandaoni la Jumia kufunga biashara yake nchini Tanzania huenda ni matokeo ya Watanzania kutokujua fursa na  elimu juu ya biashara ya mtandaoni.

Hatua hiyo ya Jumia inakuja siku chache baada ya kusimamisha oparesheni zake nchini Cameroon kusema inaangazia masoko sehemu nyingine duniani. 

Amazon hiyo ya Afrika ambayo hivi karibuni ilitangaza kuwa na watumiaji wanaotumia soko hilo mara kwa mara wapatao 5.5 milioni imefikia maamuzi hayo Novemba 27, 2019 huku na kuacha maswali mengi juu ya mstakabali wa biashara ya mtandaoni Afrika. 

Ni nchi gani kati ya hizi ambazo Jumia inaendesha shughuli zake: Nigeria, Egypt, Morocco, Kenya, Ivory Coast, South Africa, Tunisia, Algeria, Ghana, Senegal, Uganda na Rwanda ni inafuati baada ya Tanzania?

“Wakati Tanzania ikiwa na tija na tunajivunia ukuaji tulioupata kulingana na watu kutumia Jumia, tunahitaji kuelekeza rasilimali zetu kwenye masoko mengine. Maamuzi haya siyo rahisi lakini yatatusadia kuweka mitazamo na rasilimali zetu mahala zitakapoleta thamani kubwa na kusaidia ukuaji wa Jumia,” imesomeka taarifa iliyotolewa na Jumia.

Hata hivyo, huenda kufungwa kwa ofisi za kampuni hiyo nchini ikawa ni jitihada za kuipunguzia kampuni hiyo hasara kwani ripoti yake ya robo ya tatu ya mwaka huu inaonyesha kuwa ilipata hasara Sh126.5 bilioni ikilinganishwa na Sh103.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

Baadhi ya wataalam na wachambuzi wa masuala ya biashara wameiambia www.nukta.co.tz kuwa zipo sababu nyingi zinazosababisha kampuni zinazoendesha biashara ya mtandaoni sifanikiwe ikiwemo uelewa mdogo kuhusu masoko na elimu ya juu ya teknolojia ya mifumo ya kidijitali bado ni changamoto. 

Mkurugenzi wa Masoko kutoka kampuni ya masoko mtandaoni ya N-Soko,  Julius Kajuti amesema uelewa juu ya masoko ya mtandaoni ni kati ya changamoto zinazowakumba Watanzania na kuwapelekea kushindwa kuwekeza muda kwa ajili manunuzi kwa njia dijitali.

Kajuti amesema, changamoto hiyo inafanya wengi kushindwa kuamini biashara ya mtandaoni kwani wapo baadhi ya watu wanaofanya manunuzi mtandaoni lakini wanaishia kupoteza fedha zao baada ya bidhaa walizoagiza kutowafikia kwa wakati au kutofikia viwango wanavyovihitaji.

“Unakuta mtu ananunua kitu mtandaoni akitarajia kukaa nacho kwa muda mrefu lakini baada ya muda mfupi kinaharibika,” amesema Kajuti.

Mbali na hayo, masoko mengi yenye makazi yake Afrika huuza bidhaa zilizotumika na hivyo kushindwa kushindana na masoko mengine ya kimataifa ambayo bidhaa zake nyingi ni mpya.

Ni nchi gani kati ya hizi ambazo Jumia inaendesha shughuli zake: Nigeria, Egypt, Morocco, Kenya, Ivory Coast, South Africa, Tunisia, Algeria, Ghana, Senegal, Uganda na Rwanda ni inafuati baada ya Tanzania? Picha| Naija247.

Aliyewa kuwa Meneja Uhusiano wa Jumia, Godfrey Kijanga  kabla ya kampuni yake kufunga biashara aliiambia www.nukta.co.tz kuwa biashara kwa njia ya mtandao bado ni ngeni miongoni mwa Watanzania wengi kutokana na kuzoea mifumo ya asili ya manunuzi ambayo imejengeka katika jamii kwa muda mrefu.

 “Watanzania wengi bado wamekumbatia mifumo yao ya asili ya kufanya biashara na manunuzi. Wafanyabiashara bado wanategemea wateja kuja moja kwa moja madukani mwao na wateja nao bado wanaamini ili kupata bidhaa sahihi lazima uione, uiguse, uikague au kuichunguza pamoja na kuijaribu kama ikibidi,” alisema Kijanga, Agosti 2018 wakati akihojiwa na Nukta

Ikumbukwe kuwa, kufungwa kwa Jumia ni muendelezo wa kampuni kufunga biashara na kuondoka nchini kutokana na changamoto mbalimbali za utendaji na mazingira ya uwekezaji, ambayo kwa sasa Serikali inaendelea kuyaboresha ili kuvutia wawekezaji wengi.

Baadhi ya kampuni ambazo zimefungwa ni pamoja na Tala: iliyokuwa ikijushughulisha na utoaji wa mikopo kwa njia ya simu za mkononi na kampuni ya utoaji huduma za usafiri wa ndege ya FastJet.


Zinazohusiana


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Bytes ambaye pia ni Mtaalam wa masuala ya mahusiano ya umma na mitandao ya kijamii, Kennedy Mmari amekiri ni kweli Watanzania bado wana ugumu kwenye kufanya manunuzi yao mtandaoni.

“Watu hawaamini usalama wa fedha zao. Wapo Watanzania waliokumbana na changamoto kwenye majukwaa mengine kama Instagram na Facebook ambako kuna watu wanauza bidhaa. Uzoefu huo unapelekea wao kushindwa kuamini hata makampuni makubwa kama Jumia,” amesema Mmari.

Hata hivyo, Mmari amesema huenda Jumia ilijikita sana kwenye kuwekeza kwenye idara ya masoko zaidi na kusahau kutoa elimu juu ya usalama wa mfumo wake wa masoko.


Jumia siyo wa kwanza. Wapo OLX wameondoka, kupatana wao wapo lakini pia hawafanyi vizuri sana na wengine wengi tu. waliobaki ni wachache,” – Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Serengeti Bytes, Kennedy Mmari.


Nini kifanyike?

Ili kuhakikisha Watanzania wanapata elimu hiyo kwani manunuzi ya mtandaoni ndiko dunia inakoelekea, Mmari amesema ipo haja ya mamlaka zinazohusika kutoa elimu ili watu waelewe kuwa hawawezi kukwepa mwelekeo huo.

Hata hivyo, swali la urahisi na wepesi wa teknolojia huenda likawa ni changamoto kwa watumiaji wa masoko hayo linazunguka kwenye viichwa vya wadau wengi wa teknolojia.

Emmanuel Evans ambaye ni Mhandisi wa programu za kompyuta amesema haoni kama ni changamoto kwani masoko mengi ya mtandaoni hayatofautiani na akaunti za biashara za mitandao ya kijamii kama “Instagram Business” na zinginezo.

“Jukwaa kama Jumia ni rahisi kutumia kwani kuna hadi chaguo la kufanya malipo pale bidhaa yako inapokufikia. Huenda ugumu wa Watanzania ukawa kwenye hofu kwenye ubora wa bidhaa zinazonunuliwa lakini sio ugumu wa teknolojia,” amesema Evans.