July 8, 2024

Wachina wapagawishwa na mtandao kutoka Tanzania

Wauchagua mtandao uitwao Schoolbiz kuwaunganisha wajasiriamali vijana kutoka China na Tanzania.

  • Mtandao huo umelenga kuunganisha vijana na wajasiriamali katika kupata fursa mbalimbali.
  • Schoolbiz imeteuliwa kuwa kiunganishi cha fursa za kibiashara kati ya China na Tanzania.

Dar es Salaam. Jukwaa la mtandaoni la Schoolbiz Forums limechaguliwa na mkutano wa kimataifa wa wajawasiriamali uliofanyika China hivi karibuni kuunganisha wafanyabiashara kutoka China na Tanzania ili kukuza uchumi wa nchi za Afrika.

Schoolbiz ni jukwaa linalowakutanisha wanafunzi mtandaoni na kuwapa fursa ya kujifunza mambo mbalimbali na kusaidiana kutatua changamoto za ajira. 

Jukwaa hilo hufanya kazi kwa njia ya mtandao ambapo humuhitaji mwanafunzi kuingia katika tovuti, kujisajili na kisha kuanza kukutana na vijana wenzake waliokwijiunga kwa muda huo. Kujiungaa na mtandao huo huwapatia vijana nafasi ya kujadili mambo mbalimbali yatakayowasaidia katika soko la ajira na maisha kwa ujumla.

Ili kuendana na fursa mpya ya kuunganisha wafanyabiashara, Schoolbiz sasa itaongeza kipengele kitakachowahusisha wajasiriamali ndani ya mtandao huo kukutana na wenzao na kutengeneza mazingira ya kufanya kazi baina ya China na Tanzania.

Pia linawawezesha kuungana na vijana waliopo maeneo mbalimbali duniani kubadilishana uzoefu na ujuzi utakaowasaidia kuboresha maisha yao.

Hadi sasa mtandao huo una watumiaji zaidi 70 na tayari zaidi 20 wanaotumia mara kwa mara walishapata fursa za ajira.                                  Mtandao huo utakua kiunganishi cha wajasiriamali wa China na Tanzania. Picha | Kwa hisani ya Kizwalo Simbila

Jukwaa hilo la Schoolbiz lilitambuliwa rasmi kuwa kiunganishi muhimu kati ya China na Tanzania katika mkutano ulifanyika mjini Hangzhou nchini China Disemba 21, 2019 na litakuwa na shughuli ya za ziada katika biashara  zinazowagusa vijana (China-Africa Bridge Cross-Border Trade Service).

Uamuzi wa kuchagua jukwaa hilo ulikuja baada ya kubaini ufanisi wake katika kuwaunganisha vijana katika kupata fursa mbalimbali duniani hususan katika elimu. 

Pia Mkurugenzi wa mtandao huo, Kizwalo Simbila ameteuliwa kuwa Meneja wa jukwaa linalowaunganisha wajasiriamali wa Afrika na China (China-Africa entrepreneurship Forum)


Zinazohusiana:


Majukwaa mengine ya mtandaoni yaliyochaguliwa kuunganisha bara la Afrika fursa mbalimbali za kibishara nchini China yanatoka  Nigeria, Ghana na Sierra Leone.

Simbila ameiambia www.nukta.co.tz  kuwa fursa hiyo ni hatua kubwa kwa jukwaa analoliongoza kujipanua na kupata watu wengi zaidi wanaoweza kukua kiuchumi kupitia mtandao huo na fursa mbalimbali za kimataifa.

“Nimefurahi sana kuaminiwa na kupewa nafasi hiyo kwani wameona changamoto iliyopo na wakaamini inaweza kuwa fursa kwa Schoolbiz kujipanua na kuwa kiunganishi cha nchi hizi mbili kiuchumi,”amesema Kizwalo.