October 6, 2024

Wadadisi sekta isiyo rasmi Tanzania wapigwa msasa

Wametakiwa kuzingatia viwango vya ubora katika ukusanyaji wa taarifa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kubaini mahitaji na changamoto za sekta hiyo.

  • Wametakiwa kuzingatia viwango vya ubora katika ukusanyaji wa taarifa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kubaini mahitaji na changamoto za sekta hiyo.
  • NBS, ILO kufanya utafiti  kwa ajili ya kupima maendeleo ya sekta isiyo rasmi.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amewataka wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa sekta isiyo rasmi nchini kuzingatia viwango vya ubora katika ukusanyaji wa taarifa ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi zenye kubaini mahitaji na changamoto za sekta hiyo.

James aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa sekta isiyo rasmi Tanzania Agosti 4, 2019 Jijini Dar es Salaam, amesema matokeo ya utafiti huo yataisaidia Serikali kufahamu mchango halisi wa sekta isiyo rasmi katika pato la Taifa ikijumuisha ulipaji kodi.

Amesema sekta isiyo rasmi imekuwa nguzo muhimu katika kukuza pato la Taifa kwa sababu inaajiri watu wengi, kwa mujibu wa utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi uliofanyika mwaka 2014 ilibainika kuwa, asilimia 21.7 ya watu waliokuwa na ajira walikuwa katika sekta isiyo rasmi.

Amebainisha kuwa Serikali imejiwekea malengo mbalimbali katika kuinua uchumi wa wananchi wake ikiwemo kubaini changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta isiyo rasmi ikiwemo hali ya upatikanaji wa masoko, fursa za mikopo, ujuzi unaohitajika pamoja na matumizi ya teknolojia kwa nia ya kuongeza tija katika uzalishaji.

“Sina shaka na ubora wa takwimu zitakazokusanywa kwa kuwa mnaendelea kufanya kazi hii kwa karibu sana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Benki ya Dunia (WB), tumieni uzoefu wenu ili na sisi Watanzania tunufaike kuifahamu zaidi sekta hii katika kukuza uchumi wa Tanzania,” amesema James.

Kwa mujibu wa Jamues,utafiti wa kwanza wa kitaifa katika sekta isiyo rasmi Tanzania ulifanyika mwaka 1991 na kufuatiwa na utafiti kama huo katika Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 1995, hivyo ni kipindi kirefu kimepita na kufanya kuwepo na mahitaji makubwa ya takwimu zinazoakisi hali halisi ya sasa ya sekta hiyo nchini.


Zinazohusina: 


Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema hatua ya Serikali kufanya utafiti huo ni uthubutu mkubwa kwa Tanzania kwa kuwa ni nchi chache za Bara la Afrika zimeweza kufanya utafiti huo kwa ajili ya kupima sekta yenyewe na upatikanaji wa rasilimali fedha sambamba na kubaini fursa za ajira kwa wananchi.

“Kama mnayofahamu Serikali kwa sasa inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21 ambao unahitaji takwimu katika ngazi za chini za utekezaji, ili kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa lengo la kufikia lengo la angalau asilimia 40 ya watu wenye ajira ifikapo mwaka 2020” amesema Dk Chuwa.

Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na wenye Ulemavu na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imeshakamilisha maandalizi yote ya kufanyika kwa utafiti huo, unaotarajia kuanzia katika Mkoa wa Dar es Salaam Agosti hadi Novemba mwaka huu.Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (kulia) akizungumza jambo na Mwakilishi wa Benki ya Dunia Ofisi ya Dar es Salaam Ms Preet Arora (kushoto) muda mfupi baada ya kufungua mafunzo kwa wadadisi na wasimamizi wa utafiti wa sekta isiyo rasmi lAgosti 4, 2019. Katikati ni Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa pamoja na Mkurugenzi Msaidizi- Idara ya Ajira na Ukuzaji ujuzi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Muundo wa utafiti huo umegawanyika katika ngazi kuu mbili; ngazi ya ukusanyaji wa taarifa katika ngazi ya kaya na ngazi ya pili ni ngazi ya biashara (uchumi), ambapo katika ngazi ya kaya, utafiti huo umejikita katika maeneo ya taarifa za kidemokrasia, elimu, hali ya ulemavu, ajira na ukosefu wa ajira.

Dk Chuwa amebainisha kuwa sampuli ya utafiti huo katika ngazi ya kaya pia utahusisha maeneo ya kuhesabia yapatayo 200 yaliyo mkoani Dar es Salaam na kaya zilizochaguliwa zaidi ya 2,400 pamoja na ukusanyaji wa taarifa kutoka kwenye biashara zaidi ya 4,000.

Matokeo ya utafiti huo yatawezesha upatikanaji wa taarifa za kitakwimu ambazo ni wakilishi katika ngazi za Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.