October 7, 2024

Wadau wa habari wamlilia Mwanahabari Dilunga

Ni Mhariri wa gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga aliyefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wakati anapatiwa matibabu.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamhuri Media Limited, Deodatus Balile amesema mfanyakazi wake, amefariki dunia leo alfajiri (Septemba 17, 2019) kwa maradhi ya tumbo. Picha|Mtandao.


  • Ni Mhariri wa gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga aliyefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wakati anapatiwa matibabu. 
  • Awali Dilunga alikuwa mhariri wa gazeti la Raia Mwema kabla ya kujiunga na gazeti la Jamhuri mwaka huu.
  • Wadau mbalimbali wamesema alikuwa mwandishi wa habari mahiri na mwenye weledi.

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa habari nchini Tanzania wametuma salamu za rambi rambi kufuatia kifo cha Mhariri wa gazeti la Jamhuri, Godfrey Dilunga huku wakimuelezea kuwa alitoa mchango mkubwa katika tasnia ya habari nchini. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Jamhuri Media Limited, Deodatus Balile amesema mfanyakazi wake, amefariki dunia leo alfajiri (Septemba 17, 2019) kwa maradhi ya tumbo. 

Dilunga alilazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Septemba 9, mwaka huu akitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa rufaa kutokana na tatizo la maumivu ya tumbo. 

Katika taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo, Balile amesema watamkumbuka Dilunga kwa msaada alioutoa wakati anafanya kazi na gazeti la uchunguzi la Jamhuri. 

“Kwa muda mfupi aliofanya kazi Gazeti la Jamhuri, Dilunga amekuwa mtu wa msaada na ametoa mchango mkubwa katika kuboresha maudhui ya gazeti hili la Uchunguzi. Hakika pengo lake ni vigumu kuzibika,” amesema Balile

Kabla ya kujiunga Jamhuri, Dilunga aliwahi kufanya kazi na gazeti la Raia Mwema na Mtanzania miaka ya nyuma. 

Wadau mbalimbali wa tasnia ya habari wamemlilia Dilunga huku wakisema alichangia kukuza uhuru wa vyombo vya habari nchini. 

Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas katika ukurasa wake wa Twitter amesema “kwa niaba ya Serikali nimepokea kwa masikitiko kifo cha mwanahabari huyo kwa sababu aliipenda kazi yake na kuifanya kwa uaminifu.” 

Dilunga alizaliwa Oktoba 28, 1976. Ameacha mjane na watoto watatu. 


Zinazohusiana: 


Pia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Dilunga, mmoja wa wahariri na waandishi waandamizi wa habari nchini waliofanya kazi kwa ukaribu na chama hicho.

“Kimsingi alikuwa mmoja wa waandishi wa habari kwenye timu ya waandishi wa habari kutoka vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa tuliozunguka nao nchi nzima kuanzia mwaka 2000. Pumzika kwa Amani, Godfrey Dilunga,” inaeleza taarifa ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano. 

Kwa upande wake, Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kitamkumbuka marehemu Dilunga kama mwandishi wa habari makini na mhari makini aliyefanya kazi kwa weledi. 

Kampuni ya Jamhuri Media Limited imesema kwa kushirikiana na familia ya Dilunga wanaandaa taratibu za kuaga mwili hapa jijini Dar es Salaam na maziko yanatarajiwa kufanyika Morogoro alikozaliwa katika siku itakayotangazwa na familia. 

Mwili utasafirishwa kwenda Morogoro kesho Septemba 18, 2019. Kwa sasa, msiba uko Kimara Stopover kwa dada yake Dilunga. 

Dilunga aliajiriwa na kampuni ya Jamhuri tangu Februari 1, 2019 kama Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, ambapo amefanya kazi hadi mauti yalipomfika.