July 5, 2024

Wafanyabiashara walia na tozo mpya za miamala ya simu Tanzania

Wasema zimeshusha mzunguko wa fedha na zitawafanya watu kutunza fedha ndani jambo ambalo ni hatari.

  • Ni wafanyabiashara wa Mwanza wadai mzunguko wa fedha umeanza kupungua.
  • Wadai gharama za makato ziko juu kwa watu wa kawaida kumudu.
  • Wachambuzi wa uchumi washauri Serikali kuzipitia upya.

Mwanza. Siku moja baada ya tozo ya miamala ya fedha kwa njia ya simu kuanza kutumika, wafanyabiashara jijjni Mwanza wamesema zimeanza kuwaathiri ikiwemo kupungua kwa mzunguko wa fedha katika shughuli zao. 

Wafanyabiashara hao ni wale wanaojihusisha na uwakala wa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi (mobile money).

Tozo hizo zilianza kutumika  Julai 15, 2021 kwa wanaotuma au kutoa fedha kwa  simu za mkononi ambapo wanalipa kodi ya uzalendo ambayo ni kati ya Sh10 na Sh10,000 kulingana na ukubwa wa muamala.

Baadhi ya wafanyabiashara jijini hapa wanaojihusisha na uwakala wa huduma za fedha kwa njia ya simu wamesema tozo hizo siyo rafiki kwa biashara zao kwa sababu zimepandisha gharama za makato ya miamala iliyokuwa inafanyika awali.

Mathalan, kabla ya kodi hiyo, wateja wa Airtel Money walikuwa wanakatwa Sh550 kutuma fedha kwenda mtandao mwingine lakini imepanda mpaka Sh1,160. Wakitaka kutoa, watalipia Sh2,010 badala ya Sh1,400 ya awali.

Mfanyabiashara anayesambaza fedha kwenye maduka ya miamala ya fedha kwa njia ya simu (money float), Grayson Lubatula amesema toka makato ya tozo yaanze juzi mzunguko wa fedha umekuwa mdogo. 

Lubatula amesema kabla ya tozo hizo kuanza alikuwa na uwezo wa kusambaza ‘floats’ kwa maduka hayo zaidi ya 100 kwa siku lakini tangu jana biashara yake imeanza kusuasua. 

“Mzunguko wa fedha umeshuka sana,  jana sijafanya kazi kama siku za nyuma nafikiri tozo hii imekuja  kudhorotesha biashara ya fedha mtandaoni na watu sasa wataangalia namna nyingine  ya kutuma fedha kwa wapendwa wao na maduka haya ya miamala mengi yatafungwa,” amesema Lubatula wakati akiongea na Nukta Habari.

Tozo hizo ambazo zitatumika katika mwaka wa fedha 2021/22 zilipitishwa katika Bunge la Bajeti Juni mwaka huu ambapo Serikali imesema fedha zitakazopatikana katika tozo hizo zitasaidia kuboresha miundmbinu ya kutolea huduma za kijamii kama shule, zahanati na upatikanaji wa maji vijijini.

Wakala mwingine wa fedha za kwa njia ya mtandao, Anordia Fabian amesema baada ya kuwaeleza gharama hizo mpya wateja wao, baadhi wamekubali lakini wengi wao wanakataa kutoa au kutuma fedha kuepuka makato hayo. 

Amesema ni wachache wanaolazimika kutuma fedha kutokana uharaka na shida zinazowakabili lakini wanatuma kwa kulalamika. 

“Kwa siku nilikuwa na uwezo wa kuhudumia wateja zaidi ya 150 lakini toka jana hali imebadilika ni wachache mno waliofika kutoa na kutuma pesa, ” amesema Fabian.

Baadhi ya watu wamesema tozo hizo mpya zinaweza kuathiri mwenendo wa biashara na maisha ya wananchi wa kawaida. Picha| Hand International.

Amesema pamoja na malengo ya Serikali kupata fedha ili kufanya maendeleo lakini tozo hizo ni kubwa kulingana na kipato cha wananchi wa kawaida.Amesema pia itachangia vijana walioajiri kupitia kazi hizo za fedha jumuishi kupoteza au kukosa ajira. 

“Hebu fikiria zamani kutoa Sh50,000 walikuwa wanakatwa Sh2,800 lakini kwa sasa utalazimika kukatwa Sh5,000 fedha ambayo ingesaidia kununua mahitaji mengine ya nyumbani,  amesema  Jamson Bashaya mkazi wa Kirumba Mwanza ambaye alifika kutoka fedha kwenye moja ya duka  la miamala.

Bashaya amesema kwa maoni yake wanatakaothirika zaidi ni wananchi wa hali ya chini ambao huduma hizo zilikuwa zinawarahisishia biashara na kupata huduma za msingi bila kwenda benki.

Kurudi enzi za kukaa na fedha ndani

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi,  Edwin  Soko amesema tozo hizo zinaweza kuirudisha nchi enzi za kukaa na fedha ndani na hivyo kuchangia kuwepo kwa uhalifu.  

Amesema  ongezeko hilo la makato kwenye miamala ya fedha kwa njia ya simu litasababisha athari  mbalimbali za kiuchumi kwa sababu biashara hiyo iligusa watu wa kada tofauti wakiwemo watu wa hali ya chini. “Wapo watu wanaotumia miamala hii kwa ajili ya kufikisha fedha kirahisi na kutatua changamoto zao. 

Kwa  hali hii wengi wao wataachana nayo na badala yake wataanza kutumia njia nyingine mfano mtu anataka kukutumia milioni moja na yupo Magu ni bora apande gari atumie hiyo Sh4,000 kwenda na kurudi na si kutuma hiyo fedha ambayo ni zaidi ya Sh18,000 au 20,000,” amesema. 

Athari nyingine ambayo inaweza kutokea kwa mujibu wa Soko kuyumba kwa shughuli za kijamii ikiwemo huduma za matibabu.

Amependekeza Serikali kuangalia namna inavyoweza kuwafuta machozi wananchi kwa kupunguza gharama hizo kwa sababu ni sikivu.

Mchambuzi huyo amesema kama tozo hazitapungua, kuna uwezekano wa huduma za kibenki kuongezeka zaidi ingawa watakaoathirika ni wanaoishi maeneo ya vijijini ambako benki hazijafika ambao ndiyo walikuwa walengwa wa huduma hizo.

“Wategemezi wengi watashindwa kuhimili, hivyo ni vyema Serikali ikapeleka mswada wa sheria hii bungeni ili waziri mwenye dhamana akakaa na kamati yake kufanya marekebisho tozo hizi, ” amesema.