October 6, 2024

Wageni kuinufaisha Tanzania kibiashara fainali Afcon 2019

Wamiliki wa vyombo vya moto, hoteli na Serikali watapata kipato kutokana na wageni watakaoshiriki mashindano hayo yatakayofanyika kuanzia Aprili 14 hadi 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

  • Wamiliki wa vyombo vya moto na hoteli kunufaika na wageni watakaoshiriki mashindano hayo. 
  • Serikali nayo imejipanga kuweka mazingira mazuri kuongeza mapato yatokanayo na kodi za matangazo, tozo mbalimbali. 
  • Vijana washauriwa kuchangamkia fursa hiyo kupata ajira za muda mfupi.

Dar es Salaam. Wakazi wa jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani huenda wakanufaika kibiashara baada ya Serikali kusema inafanya mazungumzo na sekta mbalimbali kuangalia namna itakavytumia fursa ya wageni wataokuja kushiriki mashindano ya vijana chini ya miaka 17 katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon)hapa nchini. 

Fainali za Afcon zinatarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 14 hadi 28 mwaka huu katika viwanja vitatu;uwanja wa Taifa, Uhuru na Azam maarufu kama Chamazi Complex.

Tanzania ambayo ni mwenyeji wa mashindano hayo itawakilishwa na timu ya Taifa chini ya miaka 17 ya Serengeti Boys na kuungana na timu zilizofuzu fainali hizo za Angola, Cameroon, Guinea, Uganda, Morocco, Nigeria na Senegal.

Waziri Mkuu KassiM Majaliwa aliyekuwa akijibu maswali bungeni leo (Februari 7,2019) amesema Serikali imejipanga kupokea wageni wote wanaokuja kushiriki mashindano hayo na inaendelea na maandalizi kwa kufanya mazungumzo na kushawishi sekta zote zitakazonufaika na uwepo wa wageni hao nchini.

“Niwahakikishie watanzania kuwa ujio huu kwetu ni muhimu sana kuhakikisha tunapata mafanikio wageni hao kuingia  kuishi hapa na kurudi makwao ni jukumu letu kuhakikisha tuko salama,” amesema Majaliwa. 

Amesema Serikali tayari imeridhia mashindano hayo kufanyika hapa Tanzania na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mashindano hayo yanaleta tija kwa wananchi ina ratibiwa kwa ushirikiano wa  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),  Wizara ya Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa na wadau wengine wa mpira.   


Zinazohusiana:


Majibu hayo yametolewa na Majaliwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilolo (CCM) Venance Mwamoto ambaye alitaka kujua Serikali imejipanga vipi kutumia mashindano hayo kukuza utalii na kujitangaza zaidi kimataifa. 

Katika kuhakikisha fursa hiyo inaleta manufaa, Majaliwa amesema wanaendelea kujenga mazingira mazuri ili kupokea wageni zaidi ikiwemo kuimarisha huduma za usafiri, hoteli ili zipatikane wakati wote. 

Kupitia huduma hizo Serikali itajipatia kodi na tozo mbalimbali ikizingatiwa kuwa mapato katika kipindi hicho yataongezeka. 

“Lakini kupitia mashindano haya tumehamasisha mikoa ya jirani maeneo ambapo viwanja vitatumika na tumeambiwa viwanja vitatu vitatumika wakati wote wa mashindano Dar es Salaam na maeneo mengine shirikisho litatoa taarifa baada ya kuwa wamekamilisha maandalizi kwahiyo mikoa hiyo nayo itanufaika’ amesema.

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 cha Serengeti Boys. Picha|Mtandao.

Mashindano hayo yatakayohudhuriwa na viongozi wa juu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) akiwemo Rais wake Gianni Infantino,yatatoa ajira za muda mfupi kwa vijana ikiwemo kuuza huduma na bidhaa mbalimbali za utamaduni. 

Pia itakuwa ni fursa kwa wadau wa sekta ya utalii kutangaza shughuli zao kupitia mikutano, mabango na vipeperushi katika maeneo watakayofikia wageni na kwenye viwanja vya mpira.

Katika mashindano hayo, Serengeti Boys itafungua dimba na mabingwa mara mbili wa michuano hiyo Nigeria Aprili 14 kabla ya kupepetana na Angola Aprili 17 na kisha kukamilisha mzunguko wa kundi lake itakapokutana na Uganda Aprili 20. Kusonga mbele kwa timu kutategemea matokeo mazuri ya mchezo huo.