Wagonjwa wa saratani wazidi kuongezeka Kanda ya Ziwa
Jumla ya wagonjwa wa saratani 48,000 wamepokelewa ndani ya miaka 10 katika hospitali ya rufaa ya Bugando.
- Jumla ya wagonjwa wa saratani 48,000 wamepokelewa ndani ya miaka 10 katika hospitali ya rufaa ya Bugando.
Mwanza. Idadi ya wagonjwa wa saratani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa imekua ikiongezeka mwaka hadi mwaka ndani miaka 10 iliyopita, kasi iliyoongeza uhaba wa wodi za kulaza wagonjwa hao katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.
Saratani ni moja ya magonjwa yanayogharimu maisha ya wengi Tanzania huku yakiacha familia nyingi katika changamoto za kipato kutokana na kugharimu kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili matibabu.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali ya rufaa ya Bugando Dk Fabian Masaga amesema wakati kitengo cha kuhudumia saratani kinaanzishwa hospitalini hapo mwaka 2009 kilipokea wagonjwa 320 idadi ambayo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na kufikia wa wastani wa wagonjwa 14,000 kwa mwaka.
“Wakati huo wagonjwa walikuwa wanatibiwa kwa njia ya kemikali iliyojukana kama kwa Kiingereza kama Chemotherapy,” amesema Dk Masaga wakati akimkabidhi mkandarasi mradi wa ujenzi wa wodi ya wagonjwa wa saratani hospitalini hapo Alhamis Agosti 6.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo saratani ni tatizo kubwa kwa wakazi wa kanda hiyo ya ziwa inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Simiyu and Shinyanga.
Tangu huduma hiyo ya matibabu ya saratani ianze kutolewa mwaka 2009 hadi mwaka 2019 jumla wagonjwa 48,000 walipokelewa katika hospitali hiyo ya kanda.
Kabla ya huduma hiyo katika hospitali hiyo, wakazi wa kanda hiyo walilazimika kusafiri mpaka jijini Dar es Salaam kupata matibabu ya maradhi hayo.
Kutokana na ongezeko hilo, Dk Masaga amesema hospitali hiyo kwa sasa inakabiliwa na upungufu wa wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa wanaofika kupata matibabu hospitalini hapo.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, serikali ilijenga jengo la kusimika mashine za tiba ya mionzi lenye thamani ya Sh 5.5 bilioni ambalo limekamilika na limeanza kutumika.
Zinazohusiana:
- Mambo ya kuzingatia kukabiliana na saratani katika hatua za awali
- Wagonjwa wa saratani wahakikishiwa tiba ya kisasa ya mionzi
Mkuu wa Idara ya Saratani wa hospitali hiyo ya Bugando, Dk Nestory Masalu amesema tiba ya ugonjwa huo hutumia muda mrefu huku dawa zinazotumika ni za kemikali ambazo zinachangia kumfanya mgonjwa atapike ama kuharisha hali inayompunguzia nguvu na hivyo hulazimikakulazwa.
Amesema kutokana na umhimu huo, uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na wadau wanalazimika kujenga wodi ya kulaza wagonjwa hao yenye gorofa tatu itakayogharimu kiasi Cha Sh4 bilioni.
“Endapo fedha zitatolewa kwa wakati wodi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 na itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 120,” amesema Dk Masalu.
Amesema hospitali hiyo ina vitanda 20 vya kulaza ambavyo havitoshelezi mahitaji ya wagonjwa wanaowapokea kila siku. Idadi hiyo ya vitanda, amesema Dk Masalu, imedumu tangu mwaka 2013.
Ujenzi wa mradi huo wa wodi umefanywa kwa nguvu ya Serikali na wadau wengine.
Amesema tayari Bugando imetoa kiasi Cha Sh1 bilioni ambazo zitaanza kufanya kazi katika kipindi cha awali huku wafanyakazi wa hospitali hiyo wakijiwekea mikakati ya kuchangia ujenzi huo kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine.