July 5, 2024

Wahamiaji wabebeshwa mzigo wa Corona duniani

Wamekuwa wakinyanyapaliwa kwa kudaiwa kuwa waeneza virusi vya ugonjwa wa Corona, jambo ambalo ni kinyume na hali halisi.

  • Wamekuwa wakinyanyapaliwa kwa kudaiwa kuwa waeneza virusi vya ugonjwa wa Corona, jambo ambalo ni kinyume na hali halisi.
  • Wahamiaji na watu wenye asili ya uhamiaji wako mstari wa mbele katika vita dhidi ya COVID-19 kuliko inavyodhaniwa. 

Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limesema wahamiaji katika sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakinyanyapaliwa kwa kudaiwa kuwa wanaeneza virusi vya ugonjwa wa Corona, jambo ambalo ni kinyume na uhalisia.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM Antonio Vitorino amesema wahamiaji na watu wenye asili ya uhamiaji wako mstari wa mbele katika vita dhidi ya COVID-19 hasa katika nchi zaUingereza, Marekani na Canada. 

Bosi huyo ameeleza kuwa wakati mamilioni ya watu wakisalia majumbani kutokana na janga la COVID-19, wahamiaji wamekuwa kazini katika sekta mbalimbali muhimu kwa jamii hususan za afya na huduma za viwandani. 

“Hizo ndizo sekta ambazo wahamiaji wamebeba jukumu muhimu katika huduma za kufikisha bidhaa, huduma za usafirishaji za masoko ya chakula na  nina uhakika kwamba nyote mmeshuhudia jukumu linalofanywa na wahamiaji katika kipindi ambacho wote tumesalia majumbani tukiogopa virusi lakini wao walikuwa hapo wakifanya kazi kwa faida ya jamii nzima,” amesema Vitorino katika taarifa yake iliyotolewa wiki hii.  


Zinazohusiana.


Amebainisha kuwa hata nchini Uswisi na Italia, sehemu kubwa ya wahudumu wa afya karibu ya nusu ya wahudumu wote au asilimia 50 ni watu wenye asili ya uhamiaji au wahamiaji. 

Kwa mantiki hiyo ameitaka jumuiya ya kimataifa kutambua kuwa mchango wa wahamiaji ni mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo kwa kuwa  bila wahamiaji nchi nyingi zitataabika.