October 6, 2024

Wajue wanufaika wakubwa wa mikopo sekta binafsi Tanzania

Ripoti ya Tathmini ya Uchumi ya mwezi Desemba 2019 inaeleza kuwa sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa kwa watu binafsi au kaya ambazo zilipata wastani wa asilimia 29.9 ya mikopo yote ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizokuwa n

  • Watu binafsi waongoza kupatiwa mikopo hiyo wakifuatiwa na shughuli za kibiashara
  • Mikopo sekta binafsi imeongezeka kwa wastani wa takriban asilimia 9 katika mwaka ulioishia Novemba 2019 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

Dar es Salaam. Unaweza kusema sasa benki za biashara zimefungua milango yao baada ya mikopo kwa sekta binafsi kuongezeka kwa takriban asilimia tisa ndani ya mwaka mmoja kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo kuboresha mazingira ya biashara na sera zinazosimamia sekta ya fedha. 

Ripoti ya Tathmini ya Uchumi ya mwezi Desemba 2019 (Economic Monthly Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi karibuni inaeleza kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa wastani wa asilimia 8.9 katika mwaka ulioishia Novemba 2019 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

“Kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kulichangiwa na usimamizi thabiti wa sera ya fedha na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuboresha mazingira ya biashara,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo inayopatikana pia katika tovuti ya BoT.

​Ripoti hiyo inaeleza kuwa sehemu kubwa ya mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuelekezwa kwa watu binafsi au kaya ambazo zilipata wastani wa asilimia 29.9 ya mikopo yote ikifuatiwa na shughuli za biashara zilizokuwa na wastani wa asilimia 17.5. 

“Mikopo inayoelekezwa katika shughuli zote kubwa za uchumi imeendelea kuongezeka, isipokuwa kwa shughuli za hoteli na migahawa katika kipindi hicho,” inaeleza ripoti hiyo. 


Zinazohusiana:


Hata wakati mikopo kwa sekta binafsi ikiongezeka, riba zinazotozwa na benki za biashara nayo imeshuka kutokana na usimamizi thabiti wa sera za fedha unaofanywa na Serikali jambo ambalo ni kiasharia kizuri kwa ukuaji wa sekta ya fedha na uchumi,

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, riba iliyotozwa kwenye mikopo iliyotolewa na benki ilikuwa wastani wa asilimia 16.94 mwezi November 2019 ikishuka kutoka wastani wa asilimia 17.13 katika kipindi kama hicho 2018.

Benki kutoza riba ndogo, kunatoa fursa kwa wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao.