November 24, 2024

Wakazi Kyela wabuni mtindo mpya wa vyoo kupunguza gharama za ujenzi

Ni ule wa kujenga shimo la choo kwa mtindo wa tanuru lenye bomba dogo la kutolewa hewa.

  • Ni ule wa kujenga shimo la choo kwa mtindo wa tanuru lenye bomba dogo la kutolewa hewa.
  • Mtindo huo ni rafiki kwa jiografia ya Wilaya iliyopo kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa.
  • Licha ya kuokoa gharama kubwa za ujenzi wa vyoo, ni sababu nyingine ya magonjwa ya mlipuko.

Kyela. Ukisikia habari za Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, hutaacha kuihusisha na umaarufu wake wa kilimo cha kakao na uzalishaji wa mchele. Lakini yako mengi ambayo yanaweza kukushangaza.

Ukipita katika mitaa mbalimbali ya mji wa Kyela, kila baada ya nyumba tatu hadi nne utakutana na vitanuru vidogo vyenye bomba la plastiki juu mithiri ya majengo ya piramidi kule Misri. 

Katika hali ya kawaida unaweza kudhani ni matanuru ya kuchomea matofali au takataka, lakini ni tofauti kabisa na unavyodhani! Vitanuru hivyo ni shimo la choo ambalo hutumika kuhifadhi kinyesi. 

Mtindo huo unatajwa kuokoa gharama za ujenzi wa vyoo lakini upande wa pili umekuwa ni sababu ya wao kushambuliwa na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Katika maeneo mbalimbali nchini, tumezoea kuona shimo la choo likisakafiwa kwa zege zito na kisha kujenga juu au pembeni chumba/ kibanda kidogo cha kujisitiri wakati wa haja. Lakini kwa wakazi wa Kyela, shimo la choo hujengewa kwa matofari na kuliinua mita chache kuelekea juu na kuwekewa bomba juu la kutolea hewa.

“Hayo sio matanuru ya kuchomea matofali, ni mtindo wa vyoo huku kwetu,” anaeleza Bahati Alex, mkazi wa kata ya Ngana.

Mtindo wa vyoo unatajwa kupunguza gharama za ujenzi. Picha| Daniel Samson.

Matunuru hayo hayahitaji malighafi nyingi zaidi ya matofari, mchanga na saruji kidogo ambapo hujengwa juu ya ardhi ili kudhibiti maji yasiingie kwenye shimo hasa wakati wa mafuriko.

Mkazi wa mwingine wa kata ya Ipyana wilaya ya Kyela, Japhary Mhando anasema aina hiyo ya ujenzi wa choo ni mahususi kwa kudhibiti hewa chafu isirudi kwa watumiaji na kuwakinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

“Hilo shimo liko wazi kama tanuru fulani lakini juu lina bomba fupi kuruhusu hewa itoke juu, bila kuweka bomba choo kinanuka sana kwasababu hewa inaingia ndani ambako watu wanajisaidia. Na choo kikianza kunuka mende zinakuwa nyingi mle ndani,” anasema Mhando. 

Bomba la kutolea hewa ni uhai wa shimo lenyewe kwasababu kama hewa haitatoka nje uwezekano wa kutokea mlipuko ni mkubwa na shimo litabomoka na kutitia. “Hilo dude (shimo) kama hujaliwekea sehemu ya kupumua linapasuka kwasababu ya joto na harufu ile inaingia chooni na kinanuka sana,” anasema Mhando.

Zipo sababu mbalimbali zinazowasukuma wakazi wa Kyela kujenga vyoo kwa mtindo wa tanuru ambazo kwa kiasi kikubwa zina mahusiano ya moja kwa moja na jiografia ya wilaya hiyo ambayo sehemu kubwa ya ardhi yake ni tambarale ikiwa na miinuko michache.

Kutokana na ukweli kwamba ujenzi wa vyoo huihitaji malighafi kama mchanga, saruji, nondo, kokoto na mawe ili kujenga choo cha kisasa na imara, wakazi wengi wa Kyela hukwepa gharama hizo na kuamua kujenga vyoo vinavyoendana na uwezo wao wa kiuchumi.

Mkazi wa kata ya Mwanyanganya, Gwamaka Mwakisole anasema gharama za ujenzi wa choo ni kubwa na mtu akitaka choo cha kisasa itabidi awe na kiasi kisichopungua 600,000 kwa shimo ambalo limejengwa kwa mawe toka chini na kulifunika kwa zege ili lidumu muda mrefu.

“Watu huku ni maskini, wanachimba vyoo vifupi kama futi sita hivi na wanazungushia matofari juu yake kama tanuru,” anasema Mwakisole.


Zinazohusiana:


Pia Asili ya udongo wa Kyela ni mchanga ambao ni rahisi kuvunjika vunjika ikiwa utakutana na maji au kugandamizwa na kitu kizito. Kutokana na hali hiyo wakazi hao hujiepusha kujenga choo cha shimo kilichofunikwa kwa zege na badala yake hujenga matanuru kwa kutumia mchanga, matofari na saruji.

Mtaalamu wa Mipango Miji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Mhandisi Levi Kasitu anabainisha kuwa gharama siyo tatizo la msingi bali ni aina ya udongo ambao huvifanya vyoo vingi katika Wilaya hiyo kutitia mara kwa mara.

“Sio kwamba wanaepuka gharama, ukichimba shimo hapa katika ile hali ya mzunguko udongo unalika, kuna hali fulani ya kama mchanga mchanga ndiyo maana utakuta vyoo vingi vinatitia,” anasema Mhandisi Kasitu.

Wilaya ya Kyela iko pembezoni mwa Ziwa Nyasa na sehemu kubwa ya eneo lake ina chemichemi za maji ambazo ziko karibu na ardhi. Hiyo ina maana kuwa kina cha maji (water table) kiko juu na hata shimo la choo likichimbwa mita chache kwenda chini hukutana na maji ambayo hujaa na kuathiri udongo.

“Kitu kimoja ambacho udongo wa huku Kyela kwanza ‘water table’ iko juu na ndiyo maana wanachimba vyoo vifupi na ndio kinachosababisha vyoo kutitia. Wakati wa masika huwezi ukaenda chooni kwasababu ya maji mengi yanapanda juu,” anasema Mhandisi Kasitu.

Anabainisha kuwa sababu nyingine ni mafuriko hasa wakati wa mvua ambapo  kingo za mto Songwe na Kiwila huvunjika na maji mengi huingia kwenye makazi ya watu na kuathiri mfumo wa utoaji taka ikiwemo vyoo.

Katika kukabiliana na wingi wa maji, wakazi wa Kyela hujenga mashimo ya vyoo kwa mtindo wa tanuru ili kudhibiti maji yasiingie ndani ya shimo.

Mtindo wa kujenga tanuru dogo la kuhifadhi uchafu ni chanzo cha magonjwa ya mlipuko. Picha| Daniel Samson.

Mtindo huo unaokoa gharama lakini ni tishio kwa afya za wakazi hao

Faida mojawapo ni kwamba mtu hatalazimika kuchimba shimo la choo mara kwa mara kwasababu wakati wa mvua nyingi ambazo husababisha vyoo kufurika, maji huondoka na uchafu wote na wakati wa kiangazi hubaki vitupu.

“Ndiyo maana huwezi ukakuta vyoo vya Kyela vimejaa, wakati wa masika vyoo vinajaa lakini wakati wa kiangazi vyoo vinakuwa vitupu, maji yanashuka na uchafu,” anafafanua Mhandisi Kasitu.

Lakini mtindo huo wa vyoo umekuwa sababu kubwa ya mlipuko wa ugonjwa kama kuhara na kipindupindu, kwasababu vyoo ni vifupi na kinyesi huchanganyika na maji ya chemichemi zilizo karibu na makazi ya watu.

Muuguzi wa  zahanati ya Mkombozi iliyopo kata Mwanyanganya, Upendo George anasema mlipuko wa magonjwa hasa kipindupindu hutokea zaidi msimu wa mvua ambapo vyoo hufurika na vimelea vya magonjwa kuchanganyika na maji wanayotumia watu kwa shughuli mbalimbali.

Mazingira ya uchafu yanayosababishwa na kutapakaa kwa maji yamewafanya watu wengi hasa watoto kukumbwa na magonjwa ya kuhara, minyoo na homa za matumbo.

Mhandisi Kasitu anawashauri wakazi wa Kyela kubadili mtindo huo wa vyoo na kuchimba mashimo ambayo wanatakiwa kuyajengea kwa mawe toka chini na kuyafunika kwa zege ili visititie na kufurika wakati wa masika.

Hata hivyo, hakuna choo ambacho ni kamilifu kwa asilimia mia moja. Kila aina ya choo ina mapungufu yake lakini ni muhimu choo kiwe sehemu ya kulinda afya zetu kwa kuzingatia kanuni za usafi.