November 24, 2024

Wakulima Mbeya waikwepa mikopo ya TADB

Hiyo inatokana na kasi ndogo ya kukopa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ukilinganisha na mikoa mingine ambapo hadi kufikia Machi 2019 wakulima wa mkoa huo walikopa Sh799.99 milioni ukilinganisha na Sh102 bilioni zilizotolewa na benki hiyo.

  • Hiyo inatokana na kasi ndogo ya kukopa katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ukilinganisha na mikoa mingine. 
  • Hadi kufikia Machi 2019 wakulima wa mkoa huo walikopa Sh799.99 milioni kati ya Sh102 bilioni zilizotolewa na benki hiyo.
  • Mikopo waliyochukua wakulima wa Kagera ni mara 48 ya ile iliyochukuliwa na wakulima wa Mbeya. 
  • Amewapata changamoto ya kukopa ili waongeze mitaji ya kuendesha shughuli za kilimo.

Dar es Salaam. Rais Dk John Magufuli amesikitishwa na kasi ndogo ya  wakulima wa mkoa wa Mbeya ya kukopa mikopo katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), licha ya kuwa maarufu katika shughuli za kilimo nchini. 

Mbeya imepitwa na mikoa ya Mwanza, Lindi, Mtwara na Kagera katika kuchangamkia mikopo hiyo ambayo hutolewa kwa riba nafuu. 

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza na wakazi wa wilaya ya Kyela leo (Aprili 30, 2019) amesema licha ya Serikali kuimarisha benki hiyo  mpaka kuanza kutoa mikopo kwa wakulima nchini, mkoa wa Mbeya bado uko nyuma kuchangamkia fursa hiyo. 

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, mpaka Machi 2019, benki hiyo ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani Sh102 bilioni kwa wakulima nchini nzima.

“Ingawa nimesikitika kuona wakulima wa mkoa wa Mbeya ambao ni maarufu kwa kilimo wamekopa Sh799.99 milioni hazijafika hata Sh1 bilioni.

“Wenzenu wa Kagera wamekopa Sh38.33 bilioni, Lindi na Mtwara kwa pamoja wamekopa Sh33 bilioni na Mwanza wamekopa Sh11.25 bilioni. Mbeya ambapo ni wakulima wazuri mlizokopa hazijafika hata Sh1 bilioni,” amesema Rais Magufuli. 


Zinazohusiana: 


Kiasi hicho cha fedha ambacho wakulima wa Mbeya wamekopa ni sawa na asilimia 0.78 ya fedha zote zilizotolewa na TADB hadi Machi 2019. 

Iwapo italinganishwa kati ya mkoa na mkoa katika uchangamkiaji wa fursa za ukopaji TADB,  mikopo ilichukuliwa na wakulima wa Mbeya ni pungufu mara 48 ya fedha zilizokopwa na wakulima wa Kagera katika kipindi hicho. 

 

Dk Magufuli amesema hiyo iwe changamoto kwa wakulima wa mkoa huo ambao ni maarufu kwa kilimo kuchangamkia fursa ya kukopa katika benki hiyo ambayo mikopo yake inatolewa kwa riba ndogo ili kuboresha kilimo chao ikilinganishwa na benki nyingine za biashara. 

Mbeya ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo ambapo inasifika zaidi kwa uzalishaji wa kakao, mpunga, chai, mahindi na kahawa. 

Mathalan, ripoti ya mwaka ya utafiti wa sekta ya kilimo (AASS 2016/17) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa mkoa wa Mbeya ulishika nafasi ya tatu Tanzania bara kwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa kahawa baada ya Kagera na Ruvuma. 

Katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini, Rais Magufuli amesema Serikali imekopa mkopo kutoka Poland wa Dola za Marekani 110 milioni (Takriban Sh250 bilioni) kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kuunganisha matreka katika mji wa Kibaha mkaoni Pwani ili kuwaongezea tija wakulima. 

Rais Magufuli anaendelea na ziara yake siku nane katika mkoa wa Mbeya ambapo kesho atakuwa mgeni rasmi katika sikukuu ya Mei Mosi ambayo kitaifa itafanyika mkoani humo.