November 24, 2024

Wakulima wa pamba wanaidai Serikali Sh50 bilioni

Licha ya kwamba Serikali imelipa Sh417 bilioni kwa wakulima wa pamba, bado baadhi ya wakulima hawajalipwa pesa zao katika msimu wa mwaka 2018/2019, jambo linalowaletea changamoto ya kushiriki kikamilifu katika kilimo cha zao hilo.

  • Fedha hizo ni za malipo ya mauzo ya pamba ya msimu wa 2018/2019.
  • Sababu kubwa ni mabadiliko ya bei katika soko la dunia.
  • Serikali yasema inapambana ili wakulima walipwe fedha hizo kwa wakati. 

Dar es Salaam. Licha ya kwamba Serikali imelipa Sh417 bilioni kwa wakulima wa pamba, bado baadhi ya wakulima hawajalipwa pesa zao katika msimu  wa mwaka 2018/2019, jambo linalowaletea changamoto ya kushiriki kikamilifu katika kilimo cha zao hilo. 

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyekuwa akizungumza bungeni leo (Novemba 6, 2019) amesema mpaka sasa wakulima wa pamba wanaidai Serikali Sh50 bilioni na jitihada zinaendele kulipa fedha hizo. 

“Nikiri kwamba baadhi ya wakulima wa pamba hawajalipwa fedha zao,” amesema Bashe wakati akijibu swali la Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni aliyetaka kujua Serikali itawalipa lini wakulima hao.

Kwa mujibu wa Chegeni, hali ya wakulima kutokulipwa pesa zao kwa wakati inaweza kuwavunja moyo na kuwafanya washindwe kufanya kilimo cha zao hilo vizuri .

“Kwa mfano leo hii wakulima wa Mkoa wa Simiyu na hasa Wilaya ya Busega, wameuza pamba toka mwezi wa tano, mpaka leo hawajalipwa fedha yao,” amesema Chegeni.


Soma zaidi: 


Akitolea ufafanuzu suala hilo, Bashe amesema sababu za kucheleweshwa kwa malipo hayo ni kuwa zaidi ya asilimia 80 ya pamba huuzwa nje ya nchi na hivyo kuibua changamoto ya wanunuzi kukabiliwa na mabadiliko ya bei katika soko la dunia. 

Aidha, waziri huyo amesema Serikali bado inapambana kuhakikisha wakulima wa zao hilo wananufaika hasa ikizingatiwa kuwa, pamba ambayo imebaki mikononi mwa wakulima hadi sasa ni tani 5,000 pekee ambayo amesema itachukuliwa mwishoni mwa Novemba 2019.

Katika msimu ujao wa ununuzi wa pamba, Serikali imesema haitaingilia  kupanga bei bali itatokana na hali halisi ya soko.

“Jukumu letu kama Serikali itakuwa ni kuhakikisha mkulima hatopata hasara. Tutatafuta njia zingine za kumlinda mkulima kuliko kumuathiri mnunuzi,” amesema Bashe.