Wamiliki wa viwanda watakiwa kukata bima ya moto Tanzania
Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amewataka wamiliki wa viwanda nchini Tanzania kuhakikisha wanakata bima ili pale wanapokumbwa na ajali za moto wapate wepesi wa kulipwa fidia za mali zao.
Waziri wa viwanda na Biashara Innocent Bashungwa{aliyevaa koti} akiongea na uongozi wa kiwanda kukoboa kahawa cha Amri Amir AL-HABSSY kilichoungua kwa moto Mei 07, 2020 ambacho chanzo chake ni hitilafu ya umeme iliyotokana na radi kubwa iliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo. Picha| Waziri wa viwanda na Biashara.
- Waziri Bashungwa amesema itawasaidia wanapopata majanga ya moto.
- Amesema hayo baada ya kiwanda cha kukoboa kahawa cha Amri Al-Habssy kilichopo Karagwe mkoani Kagera kuungua.
Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amewataka wamiliki wa viwanda nchini Tanzania kuhakikisha wanakata bima ili pale wanapokumbwa na ajali za moto wapate wepesi wa kulipwa fidia za mali zao.
Bashungwa ametoa maelekezo haya baada ye kutembelea na kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Amri Al-Habssy kilichopo Karagwe mkoani Kagera kilichoungua kwa moto Mei 07, 2020 baada ya kutokea hitilafu ya umeme iliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo.
“Tunapokuwa na viwanda hatujui mambo ya kesho na keshokutwa, mambo ya ajari unaweza kupanga kila kitu lakini hakuna anayetegemea ajari itatokea muda gani, kwa hiyo kupitia kiwanda hiki nitoe wito kwa viwanda vyote nchini tuwe tunakata bima, maana kiwanda hiki kimeungua lakini walikuwa na bima ya moto,” amesema Bashungwa.
Amesema tukio kama hilo linaleta hasara kubwa siyo tu wamiliki bali wafanyakazi wanapoteza ajira zao ambazo wanategemea kujipatia kipato.
Soma zaidi:
Kufuatia kukithiri kwa matukio ya moto wilayani Karagwe, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wilaya Godfrey Muheruka imeamua kujenga kituo cha zima moto na uokoaji ambacho kitakuwa kikisaidia katika matukio ya ajali za moto pale zinapotokea.
Bashungwa amewataka wadau wa maendeleo kuchangia kituo hicho ili ujenzi wake ukamilike kwa wakati huku akichangia mifuko 200 ya saruji kwa ajili ujenzi.
Awali, meneja wa kiwanda hicho Daniel Ndayanse amesema wamepata hasara ya takriban Sh1.4 bilioni ya kuungua kwa mashine za kiwanda na mali zingine.
Kiwanda hicho kilikuwa na wafanyakazi wa kudumu 16 huajiri wafanyakazi wa msimu kati ya 800 hadi 1000 kulingana na majukumu ya kazi.
“Kiwanda chetu tulikuwa tumekiimalisha kwa kukifanya cha kisasa ambapo tuliweza kuzalisha kati ya tani 50 hadi tani 65 za kahawa safi ambazo ni takribani gunia kati ya 800 hadi 1,000 kwa saa 24 kama hakuna tatizo la umeme,” amesema Ndayanse.