November 24, 2024

Wanachokiwaza wanaume juu ya mitindo ya nywele za wanawake

Baadhi wamesema wanawake waachwe wafanye wanachokitaka kuhusu nywele zao licha ya kuona kuwa ni kiashiria cha kutokujiamini.

  • Baadhi wamesema wanawake waachwe wafanye wanachokitaka licha ya kuona kuwa ni kiashiria cha kutokujiamini.
  • Kwa wanaume, kuwa na nywele asilia ni kuukubali uzuri wako na kujiamini.
  • Hata hivyo, hayo ni maoni binafsi kutoka kwa wadau.

Dar es Salaam. “Tangu niwe na mpenzi wangu, niseme ukweli tu kuwa sijawahi kuona nywele zake. Karibia kila wiki anakua na nywele mpya, leo rasta, kesho wigi, sijawahi kushika kichwa chake nikakutana na nywele zake, ” anasema Kennedy Bundala mkazi wa Morogoro.

Katika mfululizo wa makala zilizopita tulielezea mambo mbalimbali yanayohusu nywele asilia ikiwemo namna ya kuzitunza na madhara kwa wanaotengeneza nywele za dawa. Hata hivyo, ni mara chache sana kusikia hisia au kuwaona wanaume wakijadili masuala ya nywele za wanawake kwa kina.

Je, wanaume wanawaza nini juu ya nywele za Wanawake ambao ni wake, wapenzi, mama na hata dada zao?

Bundala, ambaye amekuwa na mpenzi wake kwa mwaka mmoja na nusu sasa bila mafanikio ya kuwahi kuziona nywele zake, anasema kwa bahati mbaya hana haki yeyote ya kumpangia mpenzi wake afanye nini na nywele zake lakini siku akimuona na nywele zake atafurahi zaidi.

“Nimempenda kama livyo haijalishi awe na nywele au hata anyoe japo najitahidi kumfanya ajiamini katika hali yoyote hasa katika uhalisia wake,” analezea Bundala.

Je, nywele ni kitu kinachotiliwa maanani na mwanaume kwa mwanamke?

Mtaalamu wa masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) Jensen Kiswabi anasema wanawake wa Kiafrika ni warembo lakini huenda hawalioni hilo kwa sababu ya kudhani kuwa wanawake wa kimagharibi ni warembo zaidi na hivyo kuhitaji kuwa kama wao.



Tamaa ya kuiga umagharibi, anasema, ndiyo chanzo kikubwa cha wanawake wa Tanzania kutaka kuwa na nywele kama zao yaani nywele laini.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mwanamke ambaye ana nywele asilia ni kiashiria kuwa anajiamini.

“Nywele asili ni kiashiria kuwa unajiamini kwa jinsi ulivyo na huendeshiwi na nini watu wengine wanasema au ni kipi kinaonyeshwa zaidi kwenye vyombo vya habari,” anasema Kiswabi.

Wanaume wanawasihi wanawake waanze kuikubali asili yao badala ya kuhaha na nywele za madawa ambayo baadhi huwa na madhara kwao.

Mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam Tonny Kibadu anasema kuikubali asili yako ni jambo jema na zuri kwa kuwa anaamini nywele asilia kwa mwanamke ni kiashiria cha kujipenda na kujiamini.

Mtindo wa nywele asilia umeshika kasi lakini wanaume wana maoni tofauti. Picha|Leyla Siraj/TUDARCo.

Waachwe!

Siyo wanaume wanapenda wanawake wawe na nywele asilia bali wanataka waachwe wafanya uamuzi wao juu ya urembo wao.

Edgar Mwampinge, mkazi wa Dar es Salaam anasema mitindo ya nywele kwa wanawake ni sehemu ya urembo wao.

Pamoja na kwamba anataka wawe huru na nywele zao, Mwampinge ambaye hufanya shughuli zake tika kampuni inayohusika na kuunganisha wafanyakazi na sehemu za kufanyia kazi ya Worknasi, anasema kuna wakati huwa anawasahau watu  anaowafahamu baada ya kubadili mitindo ya nywele.

“Muda mwingine inachanganya lakini tuwaacha waendelee kufanya wanachokitaka,” anasema Mwampinge.