October 6, 2024

Wanafunzi 10 bora kitaifa kidato cha nne hawa hapa

Kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019 na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kumeupatia shangwe mkoa wa Mbeya baada ya kufanikiwa kuingiza wanafunzi sita katika orodha ya wanafunzi 10 waliofanya vizuri katika mtihani huo kitaifa

  • Ni baada ya wanafunzi sita wa mkoa huo kuingia katika orodha ya wanafunzo 10 bora kitaifa.
  • Kati ya wanafunzi wote walioingia 10 bora, saba ni wasichana
  • Sita wanatokea Shule ya Sekondari ya St. Francis Girls.

Dar es Salaam. Kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019 na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kumeupatia shangwe mkoa wa Mbeya baada ya kufanikiwa kuingiza wanafunzi sita katika orodha ya wanafunzi 10 waliofanya vizuri katika mtihani huo kitaifa.

Mbeya ambayo kupitia Shule ya Sekondari ya St. Francis Girls, imeongoza kwa kuingiza wanafunzi sita kwenye orodha hiyo ambayo kiti cha enzi kimekaliwa na mwanafunzi Joan Ritte ambaye amekuwa wa kwanza kitaifa. 

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa leo (Januari 9, 2020) na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, nafasi ya pili imeshikiliwa na Denis Kinyange kutoka Shule ya Seminary ya Nyegezi  ya mkoani Mwanza huku nafasi ya tatu pia inatokea katika mkoa katika shule ya Sengerema ikishikiliwa na Erick Mutasingwa.

Maajabu ya Mbeya yanaendelea baada ya nafasi ya nne na tano kushikiliwa na mabinti wawili kutoka shule ya St. Francis, Rosalia Mwidege na Domina Wamara.

Aliyeshikilia nafasi ya sita ni Mvano Cabangoh anayetokea Feza Boys (Dar es Salaam) huku nafasi ya saba ikirudi St. Francis Girls kwa Agatha Mlelwa akifuatiwa na mwenzake kutoka shule hiyo hiyo, Sarah Kaduma katika nafasi ya nane.

Shammah Kiunsi ambaye pia ni wa St. Francis Girls anashika nafasi ya tisa na Lucy Magashi kutoka Huruma Girls ya jijini Dodoma akifunga pazia katika orodha hiyo ya dhahabu.

Kwa matokeo hayo, mkoa wa Mbeya umeingiza shule sita ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza wenye shule mbili huku Dar es Salaam na Dodoma zikiwa na shule moja moja.


Soma zaidi:


Siri ya St. Francis kung’ara

Licha ya St.Francis kuingiza wanafunzi sita katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa, pia wanafunzi wote 91 waliofanya mtihani huo mwaka jana wamepata daraja la kwanza. 

Akiongea na Nukta (www.nukta.co.tz) leo, Mkuu wa shule ya St. Francis Girls,Mtawa Veena Vas amesema wanafunzi wake kabla ya kufanya mtihani waliahidi ushindi na wameipatia ushindi shule hiyo.

Vas amesema siyo kusoma pekee ndiyo kumeipatia shule hiyo ushindi bali nidhamu pamoja na kujituma bila mipaka ndiko kumewapatia wasichana wote wa shule hiyo ufaulu wa daraja la kwanza.

“Ufaulu kwa daraja la A shuleni kwetu ni alama 81 na hata mitihani ambayo tunayowapatia wanafunzi ni migumu. Wanapokuja kwenye ufaulu wa Necta ambao daraja la A linaanzia alam 75 inakuwa ni rahisi kwao” amesema Vas.

Pia Vas ameongeza kuwa wanafunzi wa shule hiyo wanasoma kwa makundi ili wasaidiane na kuwawezesha wote kufanya vizuri katika masomo yao. 

“Wanafunzi hawajafanya haya peke yao. Waalimu wamefanya kazi kubwa lakini pia na wazazi wametoa ushirikiano mkubwa. Wamekuwa wepesi wakiitwa shuleni kwa makosa ya kinidhamu,” amesema Vas. 

Matokeo hayo yanapatikana katika tovuti ya Necta. Ili kuyapata matokeo ya kidato cha nne mwaka 2019 bonyeza hapa. Na ya kidato cha pili bonyeza hapa.