Wanafunzi 10 bora matokeo kidato cha sita hawa hapa
Msichana Perucy Astus Mussiba kutoka shule ya Sekondari Canossa ya jijini Dar es Salaam ameongoza kitaifa.
- Perucy Astus Mussiba kutoka shule ya Sekondari Canossa ya jijini Dar es Salaam ameongoza kitaifa.
- Serikali yaingiza wanafunzi sita katika orodha hiyo.
- Mkoa wa Dar es Salaam watikisa orodha hiyo kwa kuingiza wanafunzi wanne.
Mwanza. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya kidato cha sita mwaka 2021 na kutaja wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri katika mtihani huo wakiongozwa na Perucy Astus Mussiba kutoka shule ya Sekondari Canossa ya jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde akitangaza matokeo hayo leo Jumamosi Julai 10, 2021 visiwani Zanzibar amesema Perucy aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa alikuwa anachukua mchepua wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).
Nafasi ya pili imechukuliwa na Donald Rulers Mosile kutoka shule ya Sekondari Kisimiri ya mkoani Arusha huku Cretus Amos Mihayo kutoka Tabora Boys ya Tabora akishika nafasi ya tatu.
Ismail H Mtimwa kutoka Shule ya Sekondari Kibaha ya mkoani Pwani ameshika nafasi ya nne na Olais Julius Molel kutoka shule hiyo hiyo akishika nafasi ya tano.
Nafasi ya sita imeenda kwa Geofrey Sanga wa Tabora boys huku Anorld Andrew Msanga akitawala nafasi ya saba naye kutoka Tabora Boys.
Caroline Mpale Joune kutoka Canossa ya jijini Dar es Salaam ameshikilia nafasi ya nane na nafasi ya tisa imeenda kwa John Bugeraha kutoka shule ya sekondari Feza Boys ya jijini Dar es Salaam.
10 bora kitaifa kidato cha sita imefungwa na Herry Mshana wa Feza Boys ya jijini Dar es Salaam.
Katika orodha hiyo ya dhahabu shule za Serikali na binafsi zimechuana vikali ambapo Serikali imeingiza shule sita. Mkoa wa Dar es Salaam umeibuka kidedea katika orodha hiyo baada ya kuingiza wanafunzi wanne ikifuatiwa na Tabora ambayo imeingiza watatu.
Wasichana hawajafua damu mbele ya wavulana katika orodha hiyo baada ya kufanikiwa kuingia wawili tu.