November 24, 2024

Wanafunzi vyuo vikuu waugeukia muziki kutoka kimaisha

Wadau washauri vijana wajengewe msingi mzuri wa kusoma na kuendeleza vipaji vyao wakiwa vyuoni

  •  Wanafunzi wengi bado hawatambui na kutumia hazina ya vipaji walivyonavyo.
  • Wazazi na jamii wamekuwa kikwazo kwa vijana kufikia ndoto zao.
  • Wadau washauri vijana wajengewe msingi mzuri wa kusoma na kuendeleza vipaji vyao wakiwa vyuoni 

Dar es Salaam. “Karne ya 21 ni karne ya mtu kuwa na vipaji vingi” Ni kauli ya Mkufunzi wa Chuo Kikuu Cha Tumaini (TUDARCO) kampasi ya Dar es Salaam, Richard Ngaiza kwa wanafunzi wake akiwahimiza kutumia vipaji vya vizuri.

Wanafunzi wengi wanaomaliza elimu ya juu wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la ajira, pindi wanapomaliza masomo yao na kulazimika kukaa mtaani wakisubiri kuajiriwa. Lakini wapo ambao hawasubiri kuajiriwa, wanatumia vipaji vya kujinoa na kuhakikisha vinakuwa sehemu ya kuboresha maisha. 

Ni ukweli usiopingika kuwa elimu ya chuo humuandaa mtu kwenda kuajiriwa lakini pia ni sehemu ya kuongeza maarifa na ujuzi ambao unaweza kukutengenezea mtandao wa watu wa kufanya nao kazi. 

Humphrey Moses (24) mhitimu wa Taasisi ya Usimamizi wa Kodi  (ITA) ya Jijini Dar es Salaam hakusubiri changamoto za ajira zimkute baada ya kumaliza masomo, alianza kunoa kipaji chake cha uimbaji wa nyimbo za injili. 

Moses ambaye amebobea katika fani ya Usimamizi Forodha na Kodi  amehitimu masomo yake mwaka huu (2018) huku akiamini kipaji alichozaliwa nacho mtu ndiyo silaha pekee ya kumfanikisha kijana, “Kupitia uimbaji, nimefika Nairobi Kenya na nimekutana na watu wengi waliofurahishwa na ninachokifanya.” 

Licha ya wanafunzi wengi kuwa na vipaji lakini siyo wote wenye uwezo kutambua na kutumia vyema vipaji nawalivyonavyo kutengeneza ajira zinazoweza kuleta mabadiliko katika jamii na kupunguza utegemezi.

“Kwa vijana wengi, elimu si kila kitu bali inaleta kitu” anasema Salum Nyangumwe (a.k.a Golden) msanii mwingine wa muziki wa Bongo Fleva anayechipukia.

Tangu alipojiunga na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2017/2018 hakuacha kukitendea haki kipaji chake ambapo anahangaika huku na kule kutafuta wadau watakaomwezesha kupaa zaidi katika sekta hiyo. 

Salum Nyangumwe (a.k.a Golden) mwanamziki chipuk akinoa kipaji chake. Picha| Bright Visuals

Lakini bado vijana wanaopambana kuimarisha vipaji vyao wanakutana na changamoto mbalimbali hasa wazazi ambao wamekuwa wakidai kuwa mambo wanayachagua kuyafanya hayana faida kuliko elimu wanayoipata darasani.

Safari ya Golden kufikia malengo yake katika muziki haikuwa rahisi kwasababu tangu akiwa shule ya msingi alionyesha umahiri wa kuimba lakini alipata upinzani mkubwa kutoka kwa wazazi wake. 

“Golden ameonyesha kipaji chake tangu mdogo. Kipindi alpaswa kwenda shule na madaftari mawili tuu, yeye alikuwa na matatu ambalo moja aliandikia muziki,” anasema mama yake Golden, Rachel Mwegoha, “Nilimkataza lakini ilipelekea hadi kushuka kitaaluma hivyo nikaona niwache tuu kwakua licha ya kwamba alifanya muziki, alikua vizuri darasani,”

Hata hivyo, baadhi ya wadau wa elimu wameshauri wazazi kuwasaidia watoto wao kutambua na kutumia vipaji vyao ikiwa ni njia kuongeza tija katika jamii. 

Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu Huria (OUT),Vincent Mpepo amesema hakuna shida yeyote kwa mtu kuendeleza kipaji chake huku akiwa anasoma lakini jambo la msingi la kuzungatia ni kutenga muda unaofaa kwa vitu vyote viwili ili kimoja kisimzidi mwenzie.

“Wanazuoni wa mambo ya elimu na mambo ya uandishi wa habari wanasema kitu ambacho mtu anakipenda ndicho anachokifanya kwa usahihi zaidi kuliko kitu unachomlazimisha,” amesema Mpepo

Mpepo anaamini kuwa sana hasa ya muziki haimpotezei mtu mwelekeo wa maisha bali ni mgongano wa maslahi na mmonyoko wa maadili katika jamii ambapo ameitaka jamii kuwajengea msingi mzuri wanafunzi wakiwa shuleni kufikia ndoto zao