October 7, 2024

Wanajiolojia waililia Serikali bodi ya usajili

Waiomba kuharakisha mchakato wa kuundwa kwake ili kulinda maslahi yao.

  • Waiomba kuharakisha mchakato wa kuundwa kwake ili kulinda maslahi yao.
  • Bodi hiyo itasaidia kasi ya kuendeleza rasilimali za mafuta, gesi na madini.
  • Bunge la Tanzania tayari limeanza mchakato wa kutunga sheria itakayosimamia bodi hiyo. 

Mwanza. Chama cha Wataalam wa Jiolojia Tanzania (TGS) kimeiomba Serikali kuisajili bodi itakayosimamia taaluma hiyo ilI kutoa mchango wao katika uendelezaji wa rasimali za mafuta, gesi na madini Tanzania. 

Rais wa TGS, Profesa Abdulkarim Muruma aliyekua akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Novemba 26, 2020 jijini Mwanza, amesema tangu chama hicho kianzishwe mwaka 1969 hakina usajili hali inayosababisha kushindwa kufanya kazi yao kiufanisi.

Amesema ikiwa Serikali itasikia kilio chao na kukubali kuanzishwa kwa bodi ya usajili ya wanajiolojia itawawezesha wataalam hao kutoa huduma bila vikwazo kwenye jamii na  kutengeneza fursa mbalimbali za ajira.

Pia itasaidia kutanua wigo wa uwekezaji katika sekta za madini, mafuta na gesi ambazo zikitumiwa vizuri zitasaidia kuongeza kasi ya maendeleo nchini.

“Lakini pia bodi ya usajili itasaidia kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali yanayohusiana na madini na gesi ili kukuza uchumi wa nchi,” amesema bosi huyo.


Soma zaidi: 


Tayari Bunge la Tanzania limeanza mchakato wa utungaji wa Sheria ya Bodi ya Usajili ya Wanajiosayansi ambayo itakua inasimamia shughuli zote za jiolojia ikiwemo bodi ya usajili. 

Wanajiosayansi ni wataalam waliosomea na wenye uzoefu wa fani za jiolojia (miamba), jiofizikia, jiokemia, jioteknolojia na jiolojia ya mazingira na nyinginezo.

Taaluma hizo hutolewa hapa nchini na vyuo kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amesema taaluma ya jiolojia ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa, hivyo wataendelea kushirikiana na wataalam hao kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.  

“Tunatambua mchango wa wanajiolojia katika kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta mbalimbali za madini, gesi na mafuta,” amesema Mongella.