Wananchi wapewa angalizo mradi wa maji wa Misungwi uliozinduliwa na Rais Samia
Wataalam wa mazingira wamesema ili wafaidike na mradi huo wanapaswa kutunza vyanzo vya asili vya maji kwa kuhifadhi na kupanda miti.
- Mradi huo wa Sh13.7 bilioni utatumia chanzo cha Ziwa Victoria.
- Watakiwa kutunza mazingira kwa kupanda miti na kuhifadhi uoto wa asili.
Mwanza. Wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamesema mradi wa maji wa Misungwi uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan utakuwa mkombozi kwao huku wataalam wa mazingira wakisema ili waondokane na tatizo la maji wanapaswa kutunza vyanzo vya asili vya maji kwa kuhifadhi na kupanda miti.
Juni 14, 2021 Rais wa Tanzania Samia alizindua mradi wa maji safi na usafi wa mazingira wa mji wa Misungwi wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza ambao chanzo chake ni Ziwa Victoria.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mwanza (Mwauwasa), Leonard Msenyele alisema mradi huo unaohusisha miji ya Magu na Lamadi na umegharimu Sh45.57 bilioni utawahudumia wananchi zaidi ya 64,000.
Maji yatakuwa yanatolewa ziwani na kuwekwa kwenye kisima walichokijenga kwa ajili ya kuyakusanya kisha kwenda kwenye mtambo wa kuchujia na kuyatibu.
Msenyele alisema mradi huo una pampu za maji tatu zinazoweza kuzalisha lita za maji milioni 4.7 kwa siku.
Rais Samia Suluhu Hassan azindua Mradi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Misungwi mkoani Mwanza tarehe 14 Juni, 2021. Picha| Ikulu.
Wananchi walivyoupokea mradi huo
Wakizungumza na Nukta habari (www.nukta.co.tz) wananchi wilayani Misungwi wamesema mradi huo utakuwa mkombozi kwao kwa sababu kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za uhaba wa maji katika maeneo yao.
“Hatukuwa na shida ya maji kama ilivyo sasa ambapo wananchi wanalazimika kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji umbali mrefu,” amesema Kulwa Masomi, mkazi wa kijiji cha Misungwi wilayani humo.
Mradi huo huenda ukawafaa zaidi wanawake ambao ndiyo waathirika wa ukosefu wa maji katika wilaya hiyo.
Mkazi mwingine wa Misungwi, Agnes Lukas amesema kutokana na ukosefu wa maji hulazimika kuamka saa 9 usiku kwa ajili ya kwenda kutafuta maji umbali wa kilomita 10 na njiani hukutana na wanyama wakali kama fisi.
Anasema kuzinduliwa kwa mradi huo kutasaidia kupunguza adha hiyo.
Matumaini yao yatakuwa kweli?
Wakati wakazi hao wakiwa na matumaini makubwa ya kuondokana na tatizo la maji baada ya mradi huo kukamilika, Rais Samia alitoa angalizo kuwa chanzo cha maji wanacotegemea kinaweza kisiwe endelevu kuwapatia maji ya uhakika.
“Maji haya tunayotumia sasa yanatoka kwenye chanzo kimoja ambacho ni Ziwa Victoria, endapo chanzo hiki kikakauka tutakosa sehemu nyingine ya kuchotea maji,” alisema Rais Samia katika uzinduzi wa mradi huo.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi aliwataka wananchi kuwa rafiki wa mazingira lakini pia kuanza mkakati wa kuvuna maji ya mvua na kuyahifadhi ili kusaidia kupunguza adha ya maji.
“Pamoja na kulinda rasilimali hizo, pia tuwe na utaratibu wa kuvuna maji ya mvua ambayo yatasaidia katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji lakini pia kupunguza mmomonyoka wa ardhi,”alisema Rais Samia.
Lengo la sita la Jumuiya ya Madola ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa asilimia 100. Amesema ili kufikia lengo hilo ni vema wananchi wakalinda mazingira.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akifungulia maji kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa Maji utakaohudumia Mji wa Misungwi na maeneo ya pembezoni tarehe 14 Juni, 2021. Picha| Ikulu.
Nao wataalam wa mazingira wamesema inahitajika mikakati thabiti ya kutunza mazingira hasa kudhibiti ukataji wa miti hovyo ili maji yapatikane kwa wingi.
Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Hewa Ukaa Tanzania (NCMC) Profesa Eliakimu Zahabu amewata watu kuacha kuvamia miti ya asili katika maeneo yao kwa sababu ina mchango mkubwa wa kupatikana kwa maji.
“Miti ya asili ndiyo inayolinda vyanzo vya asili vya maji, ambavyo pia hupeleka maji yake katika Ziwa Victoria, tatizo lililopo ni watu kuvamia maeneo hayo kwa kufanya shughuli zisizo halali zinazosababisha vyanzo kukauka,”amesema Prof Zahabu
Profesa huyo amewataka wananchi kushirikiana na wadau wa mazingira kuwa na kanuni ya utunzaji wa mazingira ukiambatana na kupanda miti ili kuendelea kulinda uoto wa asili.