July 5, 2024

Wanunuzi wa kahawa waonywa Kagera

Watakiwa kufuata bei elekezi ya Sh1,200 kwa kilo na kufanya biashara hiyo mchana kweupe bila kuwahujumu wakulima.

  • Watakiwa kufuata bei elekezi ya Sh1,200 kwa kilo.
  • Pia watakiwa kufanya biashara hiyo mchana kweupe bila kuwahujumu wakulima.
  • Benki ya TADB yatoa mkopo Sh7.7 bilioni kuwalipa wakulima. 

Dar es Salaam. Wakati msimu wa ununuzi wa kahawa kwa mwaka 2020/21 ukizinduliwa katika mkoa wa Kagera, wanunuzi wametakiwa kuzingatia bei elekezi ya Sh1,200 kwa kilo na kuhakikisha wanafanya biashara hiyo kwa uwazi ili kulinda maslahi ya wakulima. 

Bei hiyo elekezi itakayotumika mkoani humo ni kwa ajili ya kahawa ya maganda ambayo haijakobolewa. 

Hiyo ni tofauti na pamba ambapo Serikali imesema haitahusika kupanga bei bali nguvu ya soko itaamua.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewataka wanunuzi wa kahawa kufanya biashara hiyo mchana bila kuwahujumu wakulima kwa kuwa kahawa ni biashara halali na hakuna sababu ya kuuzwa gizani.

“Fanyeni biashara hii mchana kweupe maana hata wakulima wanavuna mchana kweupe, nielekeze tu katika mkoa wa Kagera sitaruhusu biashara ya kahawa kufanyika usiku hii siyo biashara haramu,” amesema Brigedia Jenerali Gaguti. 

Mpaka sasa, amesema wamepokea maombi ya wafanyabiashara nane na kuwataka wafanyabaiashara wengine ambao wako tayari kununua kahawa kwa bei nzuri kujitokeza na kutangaza bei ili wapatiwe kahawa.


Soma zaidi:


Mkuu huyo wa mkoa aliyekuwa akizungumza Jumanne katika Chama cha Msingi cha Mabira wilayani Kyerwa, amewataka wakulima kutunza ubora wa kahawa yao kabla ya kuipeleka katika  vyama vya msingi ili kuhakikisha kahawa kutoka Kagera inafika sokoni na ubora unaotakiwa.

Katika msimu huu 2020/21 mkoa huo unatarajia kukusanya takribani kilo milioni 60 ya kahawa juu ya kiasi cha msimu uliopita cha kilo milioni 52. 

Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Japhet Justine amesema msimu huu wa 2020/21 tayari wameweka Sh7.7 bilioni  katika akaunti za vyama vikuu vya ushirika vya KDCU Limited na KCU 1990 Limited mkoani humo kwa ajili ya kukusanya kahawa ya wakulima na bila kuchelewesha malipo yao. 

Fedha hizo ni mkopo ambao utatozwa riba ya asilimia 9 kutoka asilimia 12 iliyokuwa inatozwa awali. 

Bodi ya Kahawa Tanzania tayari imetoa tangazo la kufunguliwa kwa msimu wa ununuzi wa kahawa ambalo linatoa mambo ya msingi ya kuzingatia ikiwemo ununuzi kufanyika katika minada ya kanda.