Washitakiwa kesi ya uhujumu uchumi wafikia 10 Mwanza
Imeongezeka kutoka nane wa awali na kufikia 10 na wanashitakiwa kwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh8.6 bilioni jijini Mwanza.
- Imeongezeka kutoka nane wa awali na kufikia 10 na wanashitakiwa kwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh8.6 bilioni.
- Wapo watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na mawakili wa kujitegemea katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza.
- Wanakabiliwa makosa 95 ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza.
Mwanza. Idadi ya washitakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na mawakili wa kujitegemea imeongezeka kutoka nane wa awali na kufikia 10.
Walioongezeka katika kesi hiyo namba 10 ya mwaka 2020 ni pamoja na Anord Temba ambaye ni wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya Kipengere na aliyekuwa Meneja Uhasibu wa TPA, Japhet Jiloli.
Washtakiwa wa awali walikuwa ni Deogratius Lena, Haike Mapuli, Marystella Minja, Thomas Akile, Ibrahim Lusato, Wendline Tibuhwa na James Bedule.
Mwingine ni Wakili wa kujitegemea wa kampuni ya Mnegere ya jijini Dar es salaam Leonard Kipengele.
Washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya makosa 95 ya uhujumu uchumi.
Soma zaidi:
- Bosi Vvodacom Tanzania afikishwa mahakamni kujibu mashataka uhujumu uchumi
- Uhamiaji waeleza sababu za kuendelea kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Mwanahabari Erick Kabendera ashtakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi
Imeelezwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza kuwa kati ya January 2015 na February 2020 katika majiji ya Dar es salaam na Mwanza watuhumiwa hao walipanga njama na kuunda genge la uharifu, kutenda uharifu, kughushi nyaraka, wizi na utakatishaji wa fedha na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh8.6 bilioni
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Monica Ndyekobola amesema kulingana na aina ya makosa yaliyotajwa katika kesi hiyo, yapo yatakayokuwa na uwezo wa kusikilizwa na mahakama hiyo na mengine yatapelekwa katika mahakama za juu ikiwemo kosa la 35 hadi 65 ambayo yanayomkabili mshtakiwa wa kwanza hadi wa 8.
Awali Mawakili wa upande wa utetezi waliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ili wapate muda wa kuzungumza na wateja wao.
Kauli hiyo iliungwa mkono na wakili mwandamizi wa mashtaka, Dismas Mganyizi ambaye alisema uchunguzi bado unaendelea hivyo mahakama ipange tarehe nyingine ya kuisikiliza lakini pia mahakama iombe kibali cha kusikiliza makosa yote.
Hakimu aliridhia maombi hayo na kesi imeahirishwa hadi Julai 9 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena.