October 6, 2024

Wataalam wa uchumi washauri namna ya kuongeza mapato sekta ya madini Tanzania

Wameshauri kupitiwa kwa utekelezaji wa sheria mpya za madini na zuio la usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.

  • Wameshauri kupitiwa kwa utekelezaji wa sheria mpya za madini na zuio la usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.
  • Pia Tanzania imetakiwa kuongeza ushirikiano na jumuiya za kimataifa katik autekelezaji wasera za kodi. 

Dar es Salaam. Wataalam wa uchumi wameishauri Serikali kuchukua hatua mbalimbali kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya kodi katika sekta ya madini ikiwemo kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera na sheria za madini zilizofanyiwa mabadiliko tangu mwaka 2017.

 Watalaam hao walikuwa wakizungumza leo (Julai 26, 2019) katika mdahalo uliondaliwa na taasisi ya Policy Forum uliolenga kujadili uwazi na jinsi kuimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato katika sekta ya uchimbaji madini, mafuta na gesi. 

 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mtaalam wa Uchumi, Dk Genuine Martin amesema mabadiliko makubwa yaliyofanyika katika sekta ya madini ikiwemo uanzishwaji wa sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 yanatoa mwanga katika ukuaji wa sekta ya madini. 

 Amesema utekelezaji wa baadhi wa vipengele vya sheria na sera hizo umewafanya baadhi ya wawekezaji kufunga ofisi zao hapa Tanzania na wengine kupunguza uzalishaji, jambo linalotakiwa kuangaliwa ili kuhakikisha azma ya kuongeza mapato inafikiwa.  

“Ni vema tukaziangalia na kuzipitia sera na sheria ambazo tumezifanyia mabadiliko kama zitasaidia kuweka msingi wa kupata mapato endelevu katika sekta ya madini,” amesema Dk Martin. 


Zinahusiana: 


Hata hivyo, amebainisha kuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) apewe nguvu ya kukagua sekta ya madini ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kutokana na mfumo wa kodi uliopo katika sekta hiyo. 

 Katika siku za hivi karibuni, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alinukuliwa na vyombo vya habari kuwa wanakusudia kuanzisha mfumo wa kidijitali utakaosaidia wananchi kuipata mikataba yote ya madini. 

 Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe akichangia katika mdahalo huo amesema kuna umuhimu kwa Serikali kuelewa mfumo wa kimataifa wa kodi katika sekta ya madini ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufaidika na sekta hiyo. 

 “Nchi yetu inatakiwa kushirikiana na nchi zingine katika kuweka mifumo ya kodi inayoendana ili kupunguza changamoto zinazojitokeza kwa wawekezaji kukwepa kodi,” amesema. 

 Amesema kampuni za madini za kimataifa zinatafuta nchi yenye unafuu wa kodi na kuzikimbia nchi zenye mlundikano mkubwa wa kodi ambazo haziendani na hali ya uzalishaji. 

 Pia Serikali imeshauriwa itathmini uamuzi wake wa kuzuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (makinikia) nje ya nchi Machi, 2017 kwa sababu yameifanya ipoteze mapato ya kodi yaliyokuwa yanapatikana awali. 

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akijadiliana jambo na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mtaalam wa Uchumi, Dk Genuine Martin leo wakati wa mdahalo uliondaliwa na Policy Forum jijini Dar es Salaam. Picha|Daniel Samson.

 Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, amesema sekta ya madini inategemea zaidi upatikanaji wa taarifa sahihi hasa kutoka nchi zingine ili kufanya maamuzi sahihi ya kusimamia sekta hiyo. 

 “Serikali isaini mkataba wa kubadilishana taarifa za kodi wa kimataifa (Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters) ili kuiwezesha kupata taarifa za makampuni ya madini ya kimataifa na jinsi yanapata faida katika nchi zinakochimba madini,” ameshauri Zitto. 

Aliyewahi kuwa Mhadhiri wa UDSM, Profesa Adolfo Mascarenhas naye  amesema changamoto za Tanzania katika sekta ya madini hazitofautiana na nchi zingine za Afrika, ni vema kushirikiana na nchi hizo ili kubadilishana uzoefu na kuangalia namna ya kuongeza mapato ya kodi na mengine. 

 Washariki wengine katika mdahalo huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam wamesema ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa kodi, Serikali iunde chombo maalum kitakachokuwa kinasimamia ukusanyaji wa mapato kulingana na uzalishaji wa makampuni ya madini.