Watahiniwa 14 wafutiwa matokeo mtihani kidato cha sita 2019
Wamefutiwa matokeo hayo baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu.
- Wamefutiwa matokeo hayo baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu.
- Tisa ni watahiniwa wa shule na watano ni watahiniwa wa kujitegemea.
- Watahiniwa 20 matokeo yao yamezuiliwa baada ya kupata matatizo ya kiafya.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 14 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani ya kidato cha sita uliofanyika Mei mwaka huu.
Licha ya vitendo hivyo vya udanganyifu, ufaulu wa jumla wa katika mitihani hiyo umeongezeka kwa asilimia 0.74 kutoka asilimia 97.58 mwaka 2018 hadi asilmia 98.32 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Necta, Dk Charles Msonde aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo (Julai 11, 2019) Unguja, Visiwani Zanzibar amesema kati ya watahiniwa hao waliofutiwa matokeo, tisa ni watahiniwa wa shule na watano ni watahiniwa wa kujitegemea.
“Baraza la Mitihani la Tanzania limefuta matokeo yote ya watahiniwa 14 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani,” amesema Dk Msonde.
Idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo mwaka huu imeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana ambapo waliofutiwa matokeo kwa kuhusika na udangajifu walikuwa nane tu.
Hata hivyo, Dk Msonde hajawataja watahiniwa waliofutiwa matokeo, wala shule wanazotoka.
Soma zaidi: Ufaulu kidato cha sita waongezeka kwa asilimia 0.74
Katika hatua nyingine, Necta imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 20 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa baadhi ya masomo.
“Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani wa kidato cha sita Mei, 2020 kama watahiniwa wa shule,” amesema Dk Msonde.
Amebainisha kuwa licha ya kubainika kwa vitendo hivyo vya udangajifu, wasimamizi wa mitihani walifanya kazi kubwa ya kudhibiti vitendo hivyo visitokee kwa kuzingatia taratibu zote zilizowekwa na baraza hilo.