November 24, 2024

Watalii kutoka Ulaya vinara wa kutembelea vivutio Tanzania

Nusu ya watalii wa kimataifa wanaoingia nchini wanatoka Ulaya wakifuatia kwa mbali na mabara ya Asia na Pacific kwa asilimia 24.5.

  • Nusu (asilimia 50.8) ya watalii wageni wanatoka Ulaya wakifuatiwa kwa mbali na wanaotoka mabara ya Asia na Pacific kwa asilimia 24.5.
  • Serikali yajipanga kujitanua zaidi kuzifikia nchi za Mashariki ya Kati na Mbali.

Umewahi kujiuliza ni bara gani duniani linalotegemewa na Tanzania kupata watalii? Basi Ulaya ni bara muhimu ambalo linatoa watalii wengi wa kimataifa wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali nchini. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya utafiti wa wageni wa nje ya nchi mwaka 2017 (International Visitors’ Exit Survey Report 2017) inabainisha kuwa nusu ama asilimia 50.8 ya watalii wote wanaokuja nchini wanatoka katika bara la ulaya wakifuatiwa na mabara ya Asia na Pacific kwa asilimia 24.5.

Hata hivyo, Serikali imesema inaendelea na mipango ya kuyafikia masoko ya kimkakati ya China, Israel, Russia na Oman yanayopatikana katika eneo la Mashariki ya Kati na Mbali. 

​Utalii ni moja ya sekta zinazoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini.