November 24, 2024

Watanzania 48 kushiriki jukwaa la wajasiriamali Afrika

Ni wale wenye mawazo ya kibunifu yenye uwezo wa kutatua changamoto za jamii.

  • Ni watanzania wenye mawazo ya kibunifu kutatua changamoto za jamii.
  • Watapa mafunzo ya wiki 12 na ruzuku kuendeleza biashara zao baada ya kurudi nyumbani.

 Dar es Salaam. Watanzania wajasiriamali 48 wanatarajia kuungana na wenzao wa nchi za Afrika katika jukwaa la nne la taasisi ya Tony Elumelu Foundation (TEF) litakalofanyika Nigeria Oktoba 25 mwaka huu. 

Watanzania hao ni miongoni mwa wajasiriamali 1,000 waliochaguliwa na TEF kama watu wabunifu na wenye maandiko na mawazo ya biashara yanaweza kuleta matokeo chanya ikiwemo kutengeneza ajira kwa vijana na kupunguza umaskini barani Afrika

Jukwaa hilo litawaleta pamoja wajasiriamali, wawekezaji wa dunia, viongozi wa serikali akiwemo rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Nana Akufo-Addo (Ghana). Pia viongozi wa mashirika ya umma na binafsi, taasisi za kimataifa za maendeleo hasa zinajihusisha na masuala ya vijana. 

“Jukwaa la wajasiriamali la TEF ni tukio pekee linalowakutani wajasiriamali kutoka Afrika kuonyesha uwezo wao na serikali kuweka mazingira wezeshi ya mitaji, ushauri na muhimu zaidi ni upatikanaji wa fursa na mtandao,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa TEF,Parminder Vir OBE katika taarifa kwa wanahabari. 

TEF ilianzishwa na tajiri wa Nigeria, Tony Elumelu mwaka 2010 kwa nia ya kuchagiza ukuaji wa uchumi wa Afrika kupitia uwezeshaji wa shughuli za ujasiriamali. Kupitia TEF anakusudia kutumia Dola za Marekani 100 milioni kwa miaka 10 kuwatambua, kuwafunza na kuwawesha kwa mitaji wajasiriamali 10,000 wa Afrika. 

Lengo lake ni kuwekeza katika biashara zitakazotengeneza ajira mpya 1,000,000 na kuchangia takribani Dola 10 bilioni kwenye Pato la Mwaka la Afrika. 

 “Kwa miaka minne, tumewawezesha wajasiriamali 4,460 na tunaanza kuona matokeo ya ajira lakini muhimu zaidi tunatambua mafanikio ya kiuchumi yanaendeshwa na wajasiriamali wanawake na wanaume – ni injini ya mabadiliko ya bara letu,”  amesema Elumelu.

TEF inachagua wajasiriamali 1,000 kila mwaka kulingana na ubora wa mawazo na soko la biashara, uelewa wa mjasiriamali kwenye masuala ya fedha, uongozi na uwezo wake wa kuthibitisha ujuzi na stadi za ujasiriamali. 

Mwaka huu pekee walijitokeza waombaji 151,000 kutoka nchi 114 duniani ambapo kati ya hao 1,437 walitoka Tanzania, lakini waliofanikiwa kupita kwenye mchujo ni 48 pekee. Sekta ya kilimobiashara ndiyo iliongoza kutoa washindi wengi waliofikia 18, ikifuatiwa na TEHAMA (Teknolojia ya Mawasiliano na Habari) ambapo walikuwa 10. Na 20 waliobaki wametoka kwenye biashara ndogo ndogo, huduma za fedha, ushauri, utalii na huduma za kibinadamu. 

Baada ya kushiriki jukwaa la mwaka la TEF, wajasiriamali hao watapata mafunzo na mtaji wa Dola 10,000 kila mmoja kuendeleza mawazo ya biashara katika nchi zao. 

Baadhi ya vijana waliowahi kushiriki katika moja ya kushanyiko la TEF lililofanyika Nigeria mwaka 2017. Picha| Digest Africa

Akizungumza na Nukta, mmoja wa Wajasiriamali kutoka Tanzania ambaye amechaguliwa kushiriki katika programu ya TEF, Israel Ngoda amesema ni fursa muhimu kwake kukuza biashara na kutoa huduma za  bora kwa jamii. 

“Kuchaguliwa na programu ya TEF kuna maana kubwa sana kwangu, kwasababu kupata mafunzo ya ujasiriamali bure kwa wiki 12 pamoja na mtaji wakuendeleza biashara ni nafasi ya pekee ambayo itanisaidia kufanikisha biashara niliyoianza tayari,” amesema Ngoda.

Ngoda ambaye ni mwanzilishi wa kampuni ya Oceania inayohusika na usanifu wa tovuti na kuziwezesha biashara ndogo nchini kupitia teknolojia, amesema kupitia TEF ataweza kuifikia jamii kwa upana zaidi ikizingatiwa kuwa watajengewa uwezo wa kuboresha mawazo ya biashara, mipango na mikakati ya kuendesha shughuli za ujasiriamali kwa kiwango cha kimataifa.

“Vijana wenzangu ambao wameshaingia kwenye ujasiriamali wasikate tamaa na changamoto wanazozipitia. Wawe katika hali ya utayari pale fursa zinapotokea waweze kuzichangamkia, kusikilizia watu waliokuzidi kiuzoefu na kibiashara ili kujifunza kila siku,” amesema Ngoda.