October 6, 2024

Watanzania wafunguka ziara ya Rais Samia Kenya

Ikiwa ni siku moja tangu kukamilika kwa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Kenya, Watanzania wakiwemo wafanyabiashara wametoa maoni yao kuhusu ziara hiyo huku baadhi wakisema itafungua ukurasa mpya wa ushirikiano.

  • Baadhi yao wamesema ziara hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kimataifa.
  • Wafanyabiashara wasema ni wakati kufanya uwekezaji nchini Kenya.
  • Wananchi nao wasema imefungua upya diplomasia ya kimataifa. 

Dar es Salaam. Ikiwa ni siku moja tangu kukamilika kwa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Kenya, Watanzania wakiwemo wafanyabiashara wametoa maoni yao kuhusu ziara hiyo huku baadhi wakisema itafungua ukurasa mpya wa ushirikiano utakaowasaidia wananchi wa pande zote mbili kunufaika kiuchumi.

Rais Samia alifanya ziara ya siku nchini humo kati ya Mei 4 na 5, 2021 ambapo katika ziara hiyo alifanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili hasa katika nyanja za uwekezaji na biashara.

Katika ziara hiyo ambayo ni ya kwanza nje ya nchi kwa Rais Samia tangu ateuliwe kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka huu, alikutana na wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania na kuhutubia kikao maalum cha Bunge la Taifa na Seneti.

Sehemu ya hotuba zake alipokutana na makundi mbalimbali ilikazia kuimarisha uhusiano wa kibiashara wa nchi zote mbili na kuepuka uhasama ambao hauna faida kwa wananchi huku akiwakaribisha Wakenya kuja kuwekeza Tanzania kwa sababu ina utajiri wa rasilimali nyingi. 

Baada ya Mama Samia kukamilisha ziara hiyo na kurejea nchini, watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida wamejitokeza kutoa maoni tofauti kuhusu ziara hiyo ya kiongozi mkuu wa nchi nje ya mipaka ya Tanzania. 

Mfanyabiashara Mohammed Dewji amesema ziara ya Mama Samia nchini Kenya imempatia matumaini na faraja kama Mtanzania na kwa upande wake alichoshuhudia ni kurudishwa kwa mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

“Nina amani kubwa kwa uongozi wenye maono wa Mhe. Rais wetu Mama Samia na pia kwa kauli ya Mhe. Rais Kenyatta kwamba hatua hii siyo tu itainufaisha Tanzania bali Jumuia ya Afrika Mashariki kwa ujumla,” ameandika Dewji kupitia ukurasa wake wa Twitter.


Soma zaidi:


Ziara hiyo kwa wengine inatajwa kama ziara ya diplomasia ya biashara ambayo itafungua milango na kuimarisha shughuli za mipkani kati ya nchi hizo mbili ambazo zilikuwa haziendi vizuri kutokana na kutokuelewana kwa baadhi ya viongozi.

Wananchi wanaofanya biashara kati ya nchi hizo mbili watakuwa na uhuru wa kusafirisha huduma na biashara zao kwa uhuru huku wakiwa na uhakika wa kujipatia faida ili kuboresha maisha yao. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha kusaga unga na chakula cha mifugo, Lina Millers, Phillip Koyage amesema ziara hiyo imefungua fursa za kibiashara na kuondoa kutokuelewana ambako kulisababishwa badhi ya bidhaa za Tanzania kutokuingia Kenya yakiwemo mahindi yaliyokwama mpakani.

“Uhuru Kenyata amesema Mtanzania kufanya kazi na kuwekeza nchini Kenya hauhitaji kuwa na vibali vingi bali kufuata sheria, kwangu hii ni fursa kwani itasaidia kufikia masoko ya Kenya kwa urahisi na Afrika Mashariki kwa ujumla,” amesema Koyage.

Katika ziara hiyo, Rais Samia lipata fursa ya kutubia kikao cha Bunge la Taifa na Seneti. Picha Ikulu Mawasiliano.

Mategemeo ya mfanyabiashara huyo ni kuona Serikali ikiyafanyia kazi mambo ambayo tayari Mama Samia amekubaliana na kuyafungulia njia ili kuwafaidisha Watanzania. 

Kwa mjasiriamali na Mkurugenzi wa Shule ya kidigitali ya Assumpter, Jessica Mshama, Mama Samia anatafuta njia za kuwaondolea wafanyabiashara wa Tanzania mazowea ya kuendelea “kujifungia ndani ya boksi” kwa kuwataka waanze kupeleka biashara zao katika mataifa mengine.

Mshama ambaye ni mjasiriamali wa bidhaa za siagi ya karanga, asali na mafuta ya alizeti, amesema kuwepo kwa mahusiano mazuri ya kimasoko kati ya Tanzania na Kenya itasaidia wafanyabiashara kuongeza wigo wa masoko yao hasa kwa ngazi ya kimataifa.

Hata hivyo, baadhi ya watu wamesema Watanzania wasibwete na ziara hiyo bali waitumie vizuri kwa manufaa ya Taifa lao ili kuleta maendeleo endelevu.

Wanasiasa, wananchi nao watia neno

Baadhi ya wanasiasa wa Tanzania wamesema ziara ya mama Samia imetoa mwanga katika kuimarisha diplomasia ya kimataifa ambayo wanafikiri iliyumba na kulikosesha Taifa fursa mbalimbali za kimataifa.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, amesema ziara ya Mama Samia nchini Kenya ni sababu ya furaha kwa nchi zote mbili na imeleta matumaini ya kupanuka kwa demokrasia na uhuru wa Watanzania. 

Katika ziara yake, Rais Samia aligusia umuhimu wa viongozi hasa wanasiasa kuwa mstari wa mbele kuziunganisha nchi hizo na kuepuka migogoro ambayo haiashirii mstakabali mzuri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 

“Tabasamu la kiongozi, ni faraja tosha kwa unaowaongoza! Ahsante mama kwa Faraja hii kwetu! Hatua unazochukua kufungua uchumi wetu ni za kutia matumaini sana,” amesema Mbunge wa Mtama kwa tiketi ya CCM, Nape Nnauye. 

Kauli hiyo ya Mama Samia, baadhi ya wananchi wameichukulia kama dira ya kuifanya Tanzania kama sehemu ya kuendeleza demokrasia, siasa safi, uhuru wa watu wake usiofungamana na uadui wa vyama na makabila.

“Nimesikiliza maeneo yake hakika yanaashiria amani na utengamano wa kisiasa ikizingatiwa kuwa nchi ilipitia kipindi cha changamoto mbalimbali hasa za kisiasa,” amesema John Juma, mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye alifuatilia kwa karibu ziara hiyo.

Amesema uwezekano wa Tanzania kuwa kisiwa cha amani utakuwa mkubwa kwa sababu kiongozi wa nchi ameonyesha nia ya kushirikiana na nchi mbalimbali duniani. 

Haya hivyo, baadhi yao wamesema Tanzania inatakiwa ifanye tathmini ya kina kuhusu uhusiano huo ili kuhakikisha inafaidika zaidi.