November 24, 2024

Watanzania wamlilia Ruge kila kona

Ruge Mutahaba ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG) alifariki dunia jana nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu.

  • Ruge Mutahaba ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG) alifariki dunia jana nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu.
  • Watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, viongozi wa Serikali na wasanii wanaendelea kumuenzi kwa mchango wake alioutoa enzi za uhai wake.
  • Wengi wanamuelezea kama mtu aliyekuwa mbunifu, mzalendo wa kweli aliyefungua fursa za vijana wengi kufaidika na soko la muziki nchini.

Dar es Salaam. Watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa na wasanii wameendelea kutoa salamu za rambirambi kufuatia  kifo cha Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group (CMG), Ruge Mutahaba na kuelezea mambo mbalimbali aliyofanya enzi za uhai wake. 

Ruge, aliyezaliwa mwaka 1970 nchini Marekani, alifariki dunia jana jioni nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu na atakumbukwa zaidi kwa mchango wake mkubwa alioutoa katika tasnia za habari, muziki na kuendeleza vipaji vya vijana nchini.

Mapema jana jioni (Februari 26, 2019) Rais John Magufuli aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, “Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha kijana wangu Ruge Mutahaba. Daima nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya habari, burudani, na juhudi za kujenga fikra za maendeleo kwa vijana. Poleni wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki.”

Ruge pia mwanzilishi wa kituo cha sanaa cha Tanzania House of Talents (THT) ambacho kimewatoa wasanii wengi kama Barnaba, Mwasiti Maua Sama na Ruby. 


Soma zaidi: Wanafunzi vyuo vikuu waugeukia muziki kutoka duniani


Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amemuelezea marehemu Ruge kama kijana mbunifu na mzalendo wa kweli kwa nchi yake na ambaye alikuwa msaada mkubwa katika shughuli nyingi za maendeleo katika uongozi wake.

“Nimelemewa! Nakosa maneno ya kuelezea huzuni na majonzi niliyonayo kwa kifo cha Ruge Mutahaba. Taifa limepoteza kijana wake mahiri, mbunifu na mzalendo wa kweli. 

“Nimepoteza rafiki, mshirika mwaminifu na mtu ambaye amenisaidia kwa mengi katika uongozi wangu na hata baada ya kustaafu,” ameandika Kikwete katika ukurasa wake wa Twitter.

Mbunge wa Singida Magharibi na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambaye amefika leo nyumbani kwa baba yake Ruge kuhani msiba Mikocheni Jijini Dar es Salaam, amesema  marehemu alikuwa kijana mwenye kipaji cha pekee na kwamba atakumbukwa kwa ubunifu wake wa mawazo yaliyotoa fursa kwa vijana kupata ajira na kuendeleza maisha yao. 

Katika makala yake aliyoandika katika mtandao wa Medium, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba  amesema majonzi yake, “ni  kwamba umeondoka kabla sijalipa kwa ukamilifu deni langu kwako. Deni la upendo na urafiki wa kweli. Ulinipa heshima kubwa ya kuwa msiri wako — kwa kuniamini na kunielezea wasiwasi wako, ndoto zako, matumaini yako, harakati zako, mipango yako. Ulinipa heshima ya kunipa fursa ya kubishana nawe kuhusu mawazo na fikra zako.”

Nalo Baraza la Habari Tanzania (MCT)  limeeleza kuwa limepokea taarifa za kifo cha Ruge “kwa mshituko na majonzi makubwa”. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo (Februari 27, 2018) imeeleza kuwa  MCT imeeleza kuwa itamkumbuka kwa uthubutu wake wa kusimamia uhuru wa vyombo vya habari na uhariri, pamoja na kiu yake ya kuona tasnia ya habari inakua na inaheshimika. 

Marehemu Ruge Mutahaba akiwa na Msanii wa nyimbo za kizazi kipya, Diamond Platnumz siku za uhai wake ambapo atakumbukwa kwa mchango wake wa kukuza vipaji na kuendeleza muziki Tanzania. Picha|Mtandao.

Miongoni mwa vijana walionufaika na fursa alizotoa Ruge ni pamoja na msanii anayechipukia Rodgers Raphael ambaye pia huandikia mtandao wa Nukta. 

Raphael, ambaye alipita katika mikono ya Ruge wakati akinoa kipaji cha kuimba, amesema marehemu alithamini maoni na vipaji vya wasanii huku akisisitiza kufanya kazi kwa bidii na maarifa.  

“Alinisisitiza kufanya kazi kwa juhudi na jitihada mimi pamoja na wenzangu na kutupatia nafasi ya kushiriki kwenye majukwaa makubwa kama Urithi Festival na Mapenzi Mubashara, kitu ambacho sikuwaza kufanya hivi karibuni,” amesema Rodgers na kuongeza;

“Nitamkumbuka kwa mchango wake si tu katika muziki wangu bali  nitamkumbuka katika ukali aliouonyesha pale alipokemea uzembe katika muziki wangu, nitamkumbuka kama mtu aliyefungua njia ya watu wengi zaidi kunifahamu kama msanii mwenye matarajio.”

Wakati watu wa kada mbalimbali wakiendelea kumuenzi Ruge kwa mchango wake,  Waziri wa Habari, Utamaduni Na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amelielekeza Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) kwa kishirikiana na Jeshi la Polisi nchini kumchukulia hatua Msanii wa nyimbo za kizazi kipya Godfrey Tumaini  a.k.a Dudu Baya kwa kumdhihaki marehemu Ruge.

Katika taarifa ya Wizara iliyolewa leo, Mwakyembe amesema Dudu Baya amekuwa akitumia mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram kumdhihaki Ruge kabla na baada ya kifo chake akidai alikuwa akiwadhulumu wasanii na kumuombea afe.