November 24, 2024

Watanzania wauaga umaskini mdogo mdogo

Kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi miongoni mwa Watanzania kimeshuka hadi asilimia 25.7 mwaka 2020 kutoka asilima 26.4.

  • Kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi miongoni mwa Watanzania kimeshuka hadi  asilimia 25.7 mwaka 2020 kutoka asilima 26.4.
  • Kumechangiwa na upatikanaji wa umeme na maji, uboreshwaji wa huduma za afya na utoaji wa elimumsingi bila ada.
  • Tasaf nayo yawapiga jeki Watanzania wenye umaskini uliokithiri.

Dar es Salaam. Unaweza kusema kwa Tanzania kuingia kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati wa chini kumesaidia kuboresha maisha ya Watanzania baada ya umaskini wa mahitaji ya msingi kupungua kwa asilimia 0.7 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Mahitaji ya msingi ni pamoja na kaya au familia kupata huduma za msingi ikiwemo chakula, maji, umeme na elimu na huduma bora za afya zinazowawezesha kuishi na kufanya shughuli za maendeleo.

Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 kilichotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kimeeleza kuwa kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi miongoni mwa Watanzania hadi kufikia mwaka 2020 kilikuwa asilimia 25.7.

Kiwango hicho kimepungua kwa asilimia 0.7 kutoka asilimia 26.4 iliyorekodiwa mwaka 2018. 

Aidha, kitabu hicho kimeeleza kuwa kwa kiwango cha umaskini wa chakula pia ukipungua kutoka asilimia 8 mwaka 2018 hadi asilimia 7.3 mwaka 2020.

Kwa mujibu wa kitabu hicho, kupungua kwa viwango vya umaskini nchini kumechangiwa na upatikanaji wa umeme na maji, uboreshwaji wa huduma za afya, kuendeleza utoaji wa elimumsingi bila ada.

“Kaya maskini kuwezeshwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf),” imeeleza sehemu ya kitabu hicho ambacho kinapatikana kwenye tovuti ya NBS.

Kundi ambalo ni muhimu katika kuwakwamua wananchi kiuchumi ni wanawake ambao wanafanya biashara ndogo. Picha| K15 Photos.

Mchango wa Tasaf katika kuwakwamua Watanzania

Serikali imeendelea kuboresha hali za maisha ya watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri kupitia programu mbalimbali ikiwemo Tasaf. 

Mpango huo unatekelezwa kupitia maeneo matatu ambayo ni: kuhawilisha fedha kwa kaya maskini ili ziweze kukidhi matumizi ya kaya ikiwa ni pamoja na kuboresha lishe, kujenga uwezo wa uzalishaji na kulinda rasilimali watu.

“Kutoa ajira za muda kwa kaya za walengwa ili kuongeza kipato kwa kushiriki kufanya kazi katika miradi iliyoibuliwa na jamii; na kujenga uchumi wa kaya kwa kuhamasisha uundaji wa vikundi vya kuweka akiba, kukopeshana  na kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji mali kupitia vikundi vitakavyoundwa,” kimeeleza kitabu hicho. 

Kwa mwaka 2020, Tasaf imenufaisha kaya milioni 1.1 zenye wanufaika milioni 5.6. Kati ya wanufaika hao, wanawake walikuwa milioni 2.8 sawa na asilimia 50.8.

“Hadi Desemba 2020, Sh858.4 bilioni zilitolewa kupitia uhawilishaji fedha kwa wanufaika wote ikilinganishwa na Sh728.5 bilioni zilizotolewa mwaka 2019, sawa na ongezeko la asilimia 17.8,” kimeeleza kitabu hicho.