November 24, 2024

Watu wenye ualbino wataka kuongezewa ulinzi kuelekea uchaguzi mkuu

Licha ya mauaji kupungua, bado watu wenye ualbino wana hofu ya kushambuliwa wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

  • Licha ya mauaji kupungua, bado watu wenye ualbino wana hofu ya kushambuliwa wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
  • Wadau washauri mikakati ya kuwalinda ianze mapema kabla matukio hayashika kasi

Dar es Salaam. Licha ya matukio ya unyanyasaji na mauaji ya watu wenye ualbino kupungua nchini, bado wanakabiliwa na hofu ya kushambuliwa wakati nchi ikijiandaa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika hapo baadaye.

Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba matukio mengi ya kushambuliwa na kuuwawa kwa watu wenye ualbino hutokea zaidi kipindi cha uchaguzi ambapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakituhumiwa kutumia viungo vya watu hao katika shughuli za kishirikina.

Ripoti ya utafiti ya nusu ya mwaka ya Haki za Binadamu (Januari-June 2018), iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inaeleza kuwa licha ya juhudi za Serikali na mashirika ya kijamii kupunguza mauaji ya watu wenye ualbino bado wako katika hofu ya kushambuliwa wakati wowote.

“Watu wenye ualbino wanaendelea kuishi kwa hofu kutokana na kushambuliwa na kuuwawa kwa kukatwa viungo vya miili yao, licha ya mauaji hayo kutoripotiwa mwaka 2017 na nusu ya kwanza ya 2018,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa kuanzia mwaka huu 2018, hofu ya kushambuliwa kwa watu wenye ualbino inaweza kuongezeka ikizingatiwa kuwa takwimu zinaonyesha matukio mengi yanatokea wakati wa uchaguzi hasa wakati huu ambao Tanzania inatarajia kuingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa Urais, wabunge na madiwani utakaofanyika 2020.

Mwaka 2005 unatajwa kuwa ndiyo ulikuwa na matukio mengi zaidi ya mauaji ya watu wenye ualbino nchini ambapo takwimu  zinaonesha kwamba zaidi ya albino 70 waliuawa, zaidi ya 50 walikatwa viungo na zaidi ya 10 makaburi yao yamefukuliwa. Katika kipindi hicho ulikuwa unafanyika uchaguzi mkuu.

Mashambulizi na mauaji dhidi ya watu wenye ualbino ni kinyume cha sheria na matamko ya kimataifa kuhusu haki za binadamu ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza wazi kuwa kila mwananchi anayo haki ya kuishi. Ibara ya 14 ya Katiba hiyo inasema ‘kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa jamii kwa mujibu wa sheria’.

Wadau mbalimbali wa haki za binadamu wamejitokeza na kuitaka Serikali kuimarisha ulinzi wa watu wenye ualbino wakati huu ambao nchi inajiandaa na chaguzi ambazo zitafanyika katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), Musa Kabimba amesema kama chama wana mikakati mbalimbali kuhakikisha wanakabiliana na vitendo vyovyote vinavyolenga kuwadhalilisha watu wenye ualbino.

Kabimba ameiambia Nukta kuwa njia mojawapo wanayoitumia ni kuhakikisha usalama wa watu wenye ualbino unazingatiwa, kuelimisha jamii kuhusu athari za kuwadhuru watu wenye ualbino na kushirikiana na Serikali kuwabaini waharifu na viashiria vinavyohatarisha maisha yao.

“Kazi yetu kubwa ni kuishauri Serikali watuhakikishie usalama katika maeneo mbalimbali wakati wote, lakini pia kutoa elimu ya kutosha katika jamii zetu na ushirikiano kwa wadau wetu juu ya ukiukwaji wa sheria zinazowalinda watu wenye ualbino” amesema Kabimba.

Hata hivyo, baadhi ya watu wenye ualbino wameiambia Nukta kuwa wakati wote wanachukua tahadhari kujilinda kwa sababu mauaji ni jambo lisilotabirika.

“Sisi tunaotetea haki za watu wenye ulemavu tuko katika mazingira ya kujitahadharisha siyo tu kipindi cha uchaguzi lakini kila wakati kwa sababu matukio ni mengi yanayotokea, tunajilinda kwa kuishauri Serikali iweke mikakati rafiki kwa jili ya watu wenye ualbino nchini,” amesema Hassan Ngazi, mtetezi wa haki za watu wenye ualbino kutoka mkoa wa Morogoro.

Ripoti ya LHRC inapendekeza kuwa sheria zinazosimamia usalama wa watu ni muhimu zizingatiwe na wale wanaokiuka wachukuliwe hatua kali ili kukomesha mauaji hayo katika jamii.