October 6, 2024

Wazalishaji wa zabibu wapewa matumaini mapya Dodoma

Serikali imesema imeweka mikakati madhubuti ikiwemo uanzishwaji wa sheria mpya ya uwekezaji kumaliza changamoto zinazowakabili wawekezaji wa zao la zabibu nchni Tanzania ikiwemo utitiri wa kodi.

  • Serikali yasema itawawekea miundombinu bora ya kufanya biashara.
  • Sheria ya Uwekezaji iko mbioni kutungwa. 
  • Vijana watakiwa kuthubutu kuwekeza katika zao hilo. 

Dar es Salaam. Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri ya Mkuu anayeshughulikia  Uwekezaji Angellah Kairuki amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ikiwemo uanzishwaji wa sheria mpya ya uwekezaji kumaliza changamoto zinazowakabili wawekezaji wa zao la zabibu nchni Tanzania ikiwemo utitiri wa kodi.

Changamoto ambazo wawekezaji hao wamekuwa wakikabiliana, Kairuki amesema ni pamoja na utitiri wa kodi, ukosefu wa maji ya uhakika, ubovu wa miundombinu ya barabara, gharama kubwa za uzalishaji, uzalishaji duni kwa ubora na wingi wa zabibu, ukosefu wa aina mabalimbali za zabibu.

Pia ugumu wa kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika zabibu, ukosefu wa utaalamu katika kilimo cha zabibu, pamoja na uwepo wa bidhaa zisizo na ubora sokoni.

“Serikali inatambua changamoto mnazopitia na imeweka mikakati ya kuhakikisha inazitatua ikiwemo uanzishwaji wa sheria mpya ya uwekezaji nchini inayolenga kuweka mazingira bora ya uwekezaji,” amesema Waziri Kairuki mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma, 

Alikuwa katika ziara ya kukagua shughuli za uzalishaji katika viwanda vinavyozalisha mvivyo kikiwemo cha Domiya Estate kinachozalisha na kiwanda  cha Alko Vintages Co. Ltd. 

Waziri Kairuki amewatoa hofu wawekezaji hao kuwa maboresho ya miundombinu muhimu ikiwemo barabara, uhakika wa upatikanaji wa umeme na maji yanaendelea ili kila mwekezaji na mfanyabiashara anufaike na kuwekezaji kwake.


Soma zaidi: 


Aidha, amewataka wawekezaji kuvitumia vyema vyombo vya habari katika kutoa elimu na kujitangaza ili kuendelea kuwa na soko la uhakika kwa kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Zao la zabibu limekuwa likitegemewa zaidi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma kujipatia kipato. 

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, mwaka 2018 mkoa huo ulizalisha zabibu tani 15,017 kutoka tani 10,136 za mwaka 2015/2016. 

Hata hivyo, matarajio ni kufikisha uzalishaji wa tani 20,000 mwaka 2020/2021. 

Mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Alko Vintages Archard Kato amepongeza jitihada za Serikali za kuendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji na kuwataka vijana kutumia fursa zilizopo katika kilimo hasa cha zabibu kwa kuonesha nia na uthubuti ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

“Vijana lazima mjiamini na kuwa na uthubutu katika kuanzisha biashara ili kuingia kwenye sekta ya uwekezaji, hakikisha una maono au jambo linalokuvutia na weka mikakati ya kulifikia. Hakikisha unajaribu wazo ulilonalo na kuwatumia walioweza katika hilo, utayaona manufaa kama kijana,” amesema Kato.