October 7, 2024

Waziri atoa neno ajali ya treni Dodoma

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema Serikali itawahudumia na kuwapeleka katika maeneo yao majeruhi wote wa ajali hiyo.

  • Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema Serikali itawahudumia na kuwapeleka katika maeneo yao majeruhi wote wa ajali hiyo. 
  • Ni ile iliyotokea jana usiku baada ya treni iliyotoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam kugongana na roli karibu na stesheni ya Dodoma. 
  • Mabehewa mawili yalipinduka na kusababisha majeruhi takriban 29 waliokimbizwa hospita ya rufaa mkoa wa Dodoma.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema Serikali itawahudumia na kuwapeleka katika maeneo yao majeruhi wote wa ajali ya treni iliyotokea Jijini Dodoma, huku akiwataka wananchi kuendelea kuzingatia sheria za vivuko vya barabara na reli ili kujihakikishia usalama wakati wote. 

Ajali hiyo ilitokea jana saa 5:30 usiku ikihusisha treni la Shirika la Reli Tanzania (TRC) iliyokuwa inatoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam kugongana na roli karibu na stesheni ya Jijini Dodoma na kusababisha mabehewa mawili kupinduka na moja kuacha njia.

Katika ajali hiyo takriban watu 29 walijeruliwa na kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kupata matibabu.

Kwandikwa amewatoa majeruhi wote wa ajali hiyo kuwa watahudumia na watahakikisha wanamalizia safari zao kuelekea jijini Dar es Salaam bila usumbufu wowote.

“Niwatoe wasiwasi hata ndugu zangu ambao wako hospitali, tumejipanga tutawapa huduma kuwapeleka maeneo ambayo wanakwenda kumalizia safari zao,” amesema Kwandikwa wakati akihojiwa na Wanahabari leo Jijini Dodoma. 


Soma zaidi: Safari zote za treni ya TRC kuishia Kamata Dar


Hata hivyo, amewataka watumiaji wa barabara wakiwemo madereva kuzingatia sheria za barabarani hasa alama za reli (Railway crossing) ili kuepuka ajali wakati wakitumia vyombo vya usafiri. 

Amesema alama zimewekwa ili kuendelea kuhakikisha maisha ya watu wengine yanakuwa salama.

“Kwa watumiaji, kama unaona ajali imetokea ni kwa sababu ni sehemu ya kivuko cha reli, hivyo inapaswa mtu anayetumia gari, yule aliyegongwa na mtu yoyote tuyaangalie maeneo yale kwasababu ninaamini maeneo yale tumeyazoea kama alama za ‘railway cross’ lakini mtu anataka kupita pale bila kujali kwamba hii ni alama ya reli,” amesema Kwandikwa. 

Shughuli ya kuondoa mabehewa ya treni inaendelea huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la tukio na polisi waliokuwa na silaha. Picha|Mtandao.

Mkuu wa Stesheni Dodoma, Rose Ndauka amesema Shirika  la reli litawahudumia majeruhi wote kwa chakula na usafiri wa kurudi majumbani kwao.

Ajali kama hiyo ilitokea mwaka  2009 ambapo treni ya abiria iligongana na treni ya mizigo katika eneo la Msagali na Gulwe wilaya ya Mpwapwa katika mkoa Dodoma na kusababisha vifo na majeruhi. . 

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma, Dk Abdul Pumzi amesema majeruhi waliopokelewa wamesharuhusiwa na waliobaki hodini watawaruhusiwa  leo huku watatu wataendelea kupatiwa matibabu kwa sababu wengine wamefanyiwa upasuaji na wengine wamekutwa na shida ambazo hazihusiani na ajali hiyo.