July 5, 2024

Waziri awataka wahitimu vyuo vikuu kutafuta ajira sekta binafsi

Watakiwa kutumia vizuri ujuzi walioupata kuleta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili jamii na kutafuta ajira katika sekta isiyo rasmi ili kujiletea maendeleo.

  • Watakiwa kutumia vizuri ujuzi walioupata kuleta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili jamii.
  • Wahimizwa kutafuta ajira katika sekta isiyo rasmi ili kujiletea maendeleo.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mwanaidi Ali Khamis,  amewataka wahitimu wa vyuo vikuu Tanzania kutumia vizuri ujuzi walioupata kuleta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili jamii pamoja na kutafuta ajira katika sekta isiyo rasmi ili kujiletea maendeleo.

Khamis amesema kuwa vyuo vinatoa elimu bora ambayo kama ikizingatiwa kikamilifu inatoa fursa ya kujiajiri na kuajiriwa, hivyo kuwa chachu ya maendeleo yatakayoleta tija katika nyanja mbalimbali.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuweka mazingira mazuri ya kujiajiri hususani kwa kuboresha mazingira ya kufanya biashara na hivyo kuongeza fursa za vijana wasomi kujiajiri na hatimaye kupunguza tatizo la ajira”, amesema Khamis.

Naibu waziri huyo alikuwa akizungumza wakati wa mahafali ya 34 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika kwa mara ya 8 katika Kituo cha Kanda ya Ziwa jijini Mwanza kwa wahitimu wa shahada, stashahada na astashahada.


Soma zaidi:


Amesema kuwa baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya utoaji mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Pia kupunguza riba ya mikopo ya mabenki pamoja na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda ili kuongeza ajira na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yanayozalishwa nchini.

Amewaasa vijana wasomi kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi na kuzitumia fursa  mbalimbali zilizopo hususani katika sekta binafsi kujipatia kipato na kuwa na mchango kwa Taifa.